Simulizi

NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU -02

“Sawa! Tutashukuru sana,” alisema Anita.
Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama yule aliyekuwa akimwangalia alikuwa Edson, yuleyule mvulana aliyempenda sana tangu walipokuwa shuleni.
Hali hiyo hakutaka mumewe aione, hakutaka kugundulika ila mara nyingi alimwangalia kwa macho ya mahaba yalioonyesha kuwa na uhitaji wa kuwa na mwanaume huyo.
Baada ya dakika kadhaa, abiria walipotimia ndani ya boti, ikawashwa na safari ya kuelekea Unguja na Pemba kuanza huku Edson akiwa bize katika sehemu ya kutunza mizigo.
****
“Yule ndiye Edson mwenyewe?” aliuliza Phillip.
“Ndiye yeye! Amekwisha sana, ni vigumu kuamini kama huyu ndiye yule Edson niliyesoma naye,” alisema Anita huku akionekana kuhuzunishwa na hali aliyokuwa nayo Edson.
“Ndiyo maana nimeshangaa, jinsi ulivyoniambia na jinsi alivyo, ni vitu viwili tofauti kabisa,” alisema Phillip.
“Ndugu wamechukua kila kitu alichoachiwa na wazazi wake, anatia huruma sana,” alisema Anita.
Muda huo, boti ilikuwa safarini, ilianza safari ya kuelekea Zanzibar huku bahari ikiwa imetulia kabisa. Ndani ya boti ile kila mmoja alikuwa bize kuzungumza na mwenzake, walitegemea kutumia saa moja baharini mpaka kufika Zanzibar.
Kadiri muda ulivyozidi kwenda na ndivyo idadi ya watu waliokuwa wakipiga stori walivyozidi kunyamaza na hivyo kulala. Japokuwa Edson alilala lakini Anita hakuthubutu hata kuyafumba macho yake.
Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele juu ya mwanaume wa kwanza kuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi, Edson. Aliuhisi moyo wake kuwa kwenye mapenzi na mwanaume huyo kwani hata kipindi cha nyuma walipokuwa wameachana, hawakuachana kwa maneno wala ugomvi, waliachana kwa sababu tu masomo yaliwatenga.
Alitaka kupata nafasi ya kukaa naye na kuzungumza naye, alitaka kufahamu mengi yaliyotokea, si maisha yale aliayopitia ambayo yalijaa shida, bali alitaka kufahamu kama bado alikuwa akimpenda au la.
Alibaki kwenye kiti huku akijifikiria ni kwa namna gani angekwenda kule alipokuwa Edson na kuzungumza naye, mume wake alikuwa pembeni yake ila alikuwa amelala lakini hakuona kama ingekuwa rahisi kwake kumfuata na kupiga naye stori.
Muda ulizidi kwenda mbele, akajua kwamba endapo boti ingefika Zanzibar basi asingeweza kuzungumza na Edson, hivyo ilikuwa ni lazima aonane na mwanaume huyo hata kabla boti haijafika Zanzibar na kuachana.
“Ni lazima nikazungumze na Edson, siwezi kusubiri hapa,” alisema Anita.
Hakutaka kuendelea kusubiri, ilikuwa ni lazima akazungumze na mwanaume huyo, hakuwa tayari kujiona akisubiri zaidi, alichokifanya ni kusimama na kuanza kuelekea upande ambao ulikuwa na mizigo, sehemu ambayo ndipo Edson alipokuwepo.
Wakati anapiga hatua kuelekea huko, ghafla akashtukia tumbo likianza kuchafuka, akaanza kuyumba huku na kule na hapohapo kuanza kutapika. Hakuchukua mifuko kama abiria wengine, hivyo matapishi yake yote yakaenda chini.
Mawimbi yaliendelea kupiga huku na kule, meli ile ikaanza kuyumbishwa, kila mtu akaonekana kuogopa, bahari ilichafuka na hali ya hatari kuonekana ndani ya meli hiyo.
Haikuwa kawaida, ni kweli wakati mwingine bahari huchafuka lakini kwa siku hiyo ilikuwa zaidi. Boti ilipigwa na mawimbi mazito kiasi kwamba hata wale abiria waliokuwa wamelala, wakaamka.
Phillip aliposhtuka kutoka usingizini, mtu wa kwanza kabisa kumwangalia alikuwa mkewe, hakuwepo pale alipotakiwa kuwepo, akajaribu kuangalia huku na kule lakini hakumuona, si yye tu bali hata mtoto, naye hakuwepo.
Alichanganyikiwa, hakutaka kubaki mahali pale, tayari abiria walianza kupiga kelele za kutaka kuokolewa kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana hakukuwa na dalili kwamba wangebaki salama kabisa.
Phillip akatoka nje ya sehemu aliyokuwa amekaa na kuanza kuangalia huku na kule, alipoona kwamba mkewe hamuoni, akaanza kuita huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Anita…Anita…” aliita huku akiangalia huku na kule lakini hakuweza kumuona mkewe.
Watu wakaanza kukimbia huku na kule kwa kuamini kwamba wangeweza kuyaokoa maisha yao lakini hilo halikuwafanya kutoka nje ya meli, walibaki mule mule.
Mawimbi mazito yaliendelea kuipiga boti ile, katika hali ya kushangaza, maji yakaanza kuingia ndani ya boti ile hali ilizidi kumtia hofu kila abiria.
“Tusaidieni tunakufaaaa…” alisema abiria mmoja.
Hali ikawa mbaya, mawingu mazito yakaanza kujikusanya angani na wala hazikupita dakika nyingi, mvua ikaanza kunyesha. Ndani ya meli hakukukalika, kila mmoja alikuwa akihangaika kuyaokoa maisha yake.
Anita pale alipokuwa alikuwa kwenye hali mbaya, alijitahidi kusimama ili kurudi alipotoka lakini hakuweza, boti ilikuwa ikiyumbayumba sana kutokana na kupigwa na mawimbi.
Maji yaliendelea kuingia ndani ya boti, nahodha na wafanyakazi wengine walijitahidi kutafuta mawasiliano ya simu lakini hayakupatikana kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya.
Baada ya dakika kumi, boti ikaanza kuzama kutokana na maji mengi kuingia ndani. Hakukuwa na maboya ya kutosha hivyo abiria wengi kuhofia kufariki dunia ndani ya boti ile.
“Tunakufaaa…” walisema abiria katika kipindi ambacho boti iliendelea kuzama.
Hakukuwa na mtu aliyemsaidia mwenzake, walikuwa katikati ya bahari, katika kila upande, hakukuonekana kuwa na dalili za nchi kavu, hakukuwa na aliyejua pande za dunia yaani Kusini ilikuwa wapi na Kaskazini ilikuwa wapi.
Boti ilizama, abiria wenye ujuzi wa kuogelea wakaanza kuogele kwa staili ya kulegeza miili yao na kubaki juu wakielea, kwa wale ambao hawakuwa na uwezo wowote ule, wakaanza kuzama na kufa huko baharini.
Wakati boti ikizama, Edson alikuwa katika chumba cha mizigo. Kwa jinsi boti ile ilivyokuwa ikiyumbishwa, hali iliyokuwepo baharini alijua kwamba kulikuwa na hatari ya boti kuzama humo baharini, alichokifanya ni kuelekea nje.
Huko, hapohapo akaanza kumtafuta Anita, alijua kwamba msichana huyo hawezi kuogelea hivyo hakutaka kuona akifa, alimpenda kwa moyo mmoja, aliendelea kumtafuta zaidi.
Mpaka boti inaanza kuzama, hakuwa amemuona Anita. Alijitahidi kuita huku na kule, tena kwa sauti kubwa lakini hakusikia msichana huyo akiitikia, moyo wake ulimuuma mno.
Kwa kuwa alikuwa na ujuzi wa kuogelea, akaanza kuogelea na kumtafuta Anita. Kila alipopita, watu walikuwa wakilia na kuomba msaada. Hakutaka kumsaidia mtu yeyote yule, kwa wakati huo, mawazo yake yalikuwa kwa Anita tu. Alikuwa akimtafuta kwa kupiga mbizi huku na kule.
Ndani ya dakika tano nzima tangu boti izame, hakuweza kumuona Anita.
****
Maji yaliingia ndani ya boti na hivyo kuanza kuzama. Anita alipiga kelele za kuomba msaada huku mkononi akiwa na mtoto wake lakini hakukuwa na mtu aliyemsaidia, kila mmoja alikuwa bize kuyaokoa maisha yake lakini si kumsaidia mtu mwingine.
Mbele yake alikiona kifo, hakuwa na uhakika kama angepona, kwake, alijua kwamba ilikuwa ni lazima kufa, hivyo akaanza kusali sala yake ya mwisho na kuyakabidhi maisha yake na ya mtoto wake mikononi mwa Mungu.
Boti ilipozama, hakukuwa na msaada wowote ule, alikuwa radhi kunywa maji lakini si kuona maji yakimuua mtoto wake, hivyo alijitahidi kumshika kwa mkono mmoja na kumpeleka juu huku miguu yake ikifanya kazi ya kukata maji ili asizame.
Wakati akiwa kwenye harakati za kujiokoa yeye na kumuokoa mtoto wake, akaanza kusikia akiitwa jina lake. Kitu cha kwanza akaisikiliza sauti ile kwa makini, alichohisi ni kwamba alikuwa akiitwa na mumewe, Phillip lakini alipoisikia vizuri sauti ile, haikuwa ya mumewe bali ilikuwa ni ya aliyekuwa mpenzi wake, Edson.
“Anita…..Anita…Anita….” iliendelea kusikika sauti ya Edson.
“Edson…Edson nisaidie naku…” alisema Anita lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake akaanza kunywa maji.
Japokuwa kulikuwa na kelele mahali hapo lakini Edson aliweza kuisikia sauti hiyo, alijua ilipotokea hivyo kuanza kupiga mbizi kuelekea kule sauti ilipotokea.
Alipofika huko, akaanza kuangalia huku na kule, tayari watu wengine walikuwa wamekufa, miili yao ilielea hivyo watu wengine kuishikilia miili hiyo ili wasizame.
Edson alipomuona Anita, hapohapo akaanza kumsogela, alipomfikia, kitu cha kwanza akamchukua Cynthia.
“Vipi Anita?” aliuliza Edson.
“Ninakufa Edson, ninakufaaaa.”
“Huwezi kufa! Hautoweza kufa. Kama utakufa, basi acha na mimi nife,” alisema Edson huku macho yake tu yakionekana kumaanisha alichokisema.
Alichokifanya, mkono mmoja ukamshikilia mtoto Cynthia aliyekuwa akilia huku akipiga mbizi na kumwambia Anita amfuate kule alipokuwa akielekea. Safari yao fupi iliishia sehemu iliyokuwa na pipa moja kubwa lililokuwa likielea na kumwambia Anita alishikilie pipa hilo kwani ndiyo ulikuwa msaada pekee waliokuwa nao.
ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA KUMBUKA KUSHARE

Facebook Comments

Tags
Show More

Related Articles

Close