Simulizi

Niliua Kumlinda Mama Yangu -03


Alichokifanya, mkono mmoja ukamshikilia mtoto Cynthia aliyekuwa akilia huku akipiga mbizi na kumwambia Anita amfuate kule alipokuwa akielekea. Safari yao fupi iliishia sehemu iliyokuwa na pipa moja kubwa lililokuwa likielea na kumwambia Anita alishikilie pipa hilo kwani ndiyo ulikuwa msaada pekee waliokuwa nao.
Watu wengine waliendelea kufa, kelele zilianza kupungua kwani pamoja na kuwa kwenye hali mbaya, mvua ile iliyokuwa ikiendelea kunyesha ikasababisha baridi kali lililowamaliza watu wengi baharini hapo.
Alichokifanya Edson ni kumshikilia vizuri Cythia, akamwambia Anita ajitahidi akae juu ya pipa lile kwani ndiyo ingekuwa nafasi pekee ya kuyaokoa maisha yake.
Alichokifanya Anita ni kuanza kupanda pipa lile. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo, alijitahidi sana kupanda, alitumia muda wa dakika kumi nzima ndipo akafanikiwa na hivyo kuwa juu ya pipa lile kisha Edson kumpa Cynthia.
“Na wewe panda!”
“Hapana Anita! Sitoweza kupanda.”
“Nashukuru kwa msaada wako Edson, nashukuru kwa kuokoa maisha yangu,” alisema Anita huku akimwangalia Edson usoni.
“Usijali! Nimefanya hivi kwa kuwa ninakupenda sana Anita. Siku zote nimekuwa nikikufikiria, sikujua ni kwa namna gani ningeweza kukuona tena,” alisema Edson huku akimwangalia Anita.
Huo haukuwa mwisho, waliendelea kukaa baharini mpaka ilipofika jioni ya saa kumi na mbili ndipo kwa mbali walipoona Boti ya Mv Space ikiwa inakaribia kule walipokuwa.
Walikuwa kwenye hali mbaya, baridi liliwapiga na njaa ziliwauma mno. Kuna kipindi walifikiria kwamba hata Cynthia alikufa kwani alikuwa kimya kabisa hali iliyomfanya mara kwa mara Anita kumtingisha, alipoona akianza kulia, alimuacha.
“Edson…Edson…boti,” alisema Anita kwa sauti ya chini, alikuwa akimwamsha Edson aliyeonekana kuwa kwenye mawazo mengi.
“Unasemaje?” aliuliza Edson huku akitetemeka, nusu ya mwili wake ilikuwa majini.
“Boti…”
Aliposikia neno boti akapata nguvu na kuona kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yao ya kuokolewa. Akatupia macho kule alipoambiwa kwamba kulikuwa na boti, kweli aliiona ikiwa inasogea kule walipokuwa.
Alichokifanya ni kupunga mkono wake mmoja huku akipiga kelele za kuomba msaada. Hiyo ilionekana kusaidia kwani watu waliokuwa kwenye boti ile waliamua kuzungukazunguka katika eneo lile boti ilipozama ili kuona kama kuna majeruhi basi wawasaidie kwani hali ilionekana kuwa mbaya.
“Tupo haiiiii….tupo haiiiiii….” alipiga kelele Edson.
Hiyo ilisaidia kwa kiasi kikubwa, watu wale waliokuwa kwenye boti ile walipoisikia sauti ya Edson, wakaanza kuangalia kule sauti hiyo ilipotoka, kwa bahati nzuri wakamuonaAnita akiwa juu ya pipa, kwa pembeni alikuwepo mwanaume mwingine.
“Wale kule…” alisema mwanaume mmoja na hivyo kusogea kule kisha kuwatupia boya lililofungwa kamba, walipolishika, wakaanza kuwavuta. Huo ndiyo ukawa msaada kwao.
****
Taarifa zilitolewa katika vyombo vya habari hasa redio na televisheni kwamba boti moja ya Royal Palm ambayo ilikuwa ikifanya safari zake kwenda Unguja na Pemba ilipata ajali na abiria wengi kufariki.
Kila mtu aliyesikia taarifa hiyo, alisikitika, wengine hasa waliokuwa na ndugu zao wakalia na kuomboleza kwa kujua kwamba wasingeweza kuwaona tena ndugu wao hao.
Miili ya watu waliokufa katika ajali hiyo ikaokolewa na kupelekwa hospitalini ambapo huko watu walitakiwa kwenda ili kuona kama kulikuwa na ndugu zao hivyo kuichukua miili hiyo na taratibu nyingine kufuata.
Mtu ambaye alikuwa mmoja wa watu waliofika hospitali na kuiangalia miili hiyo alikuwa Anita na baadhi ya ndugu zake. Alifika hapo kwa ajili ya kuutafuta mwili wa mume wake aliyempenda, Phillip.
Walipelekwa katika chumba kilichokuwa na miili hiyo, walifunuliwa miili yote na kuonyeshewa, hakukuwa na mwili wa Phillip kitu kilichoonyesha kwamba mume wake huyo alikufa na mwili wake kuliwa na samaki.
“Miili ndiyo hii tu?” aliuliza Anita huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo hii tu! Hakuna mingine.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Lakini subiri kwanza,” alisema daktari mmoja.
Akaondoka na kuwaacha watu hao wakiwa katika mabenchi hospitalini hapo wakilia tu. Anita alimuomba Mungu ili amfanikishe kumuona mume wake na hata kama hatomuona basi angeridhika zaidi kama angeuona mwili wake tu.
Ndugu zake wakajaribu kumbembeleza lakini hakunyamaza, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, hakutaka kusikia la mtu yeyote yule, kile alichotaka kukisikia ni kuhusu mume wake tu.
Daktari yule aliporudi, wakasimama na kumsogelea, walitaka kusikia kile kilichotokea kule alipokwenda kama aliweza kumuuona mwili wa Phillip au la.
“Vipi?”
“Huko nilipokwenda wamesema kwamba miili ya wahanga wa ajali ya boti ni hii tu,” alisema daktari yule.
Kilio zaidi kikaanza kusikika kutoka kwa Anita, hakuamini kama kweli huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kumuona mume wake mpendwa. Alibaki akiwa na maumivu mazito moyoni mwake, huzuni aliyokuwa nayo haikuweza kusimulika.
Alilia na kulia lakini ukweli ulibaki palepale kwamba mwili wa mume wake haukuwepo na kulikuwa na uwezekano kwamba ulilikuwa na samaki huko baharini.
Kilichofuata baada ya hapo ni kuweka mazishi, watu wengi walikwenda katika msiba huo mzito. Kilio cha Anita kilimhuzunisha kila mtu aliyekuwepo mahali pale, alilia kwa kulalamika kwamba Mungu aliamua kumuonea kwani hata mwili wake ungekuwa umepatikana, kwake ingekuwa faraja kubwa mno.
Baada ya saa kadhaa, jeneza likaletwa, padri akasimama na kuomba sala maalumkisha safari ya kuelekea makaburini kuanza.
Ndani ya jeneza lile hakukuwa na mwili wake, kulikuwa na nguo zake tu na baadhi ya vitu alivyokuwa navyo. Phillip alifariki kwa maana hiyo mali zote alizokuwa nazo, ule utajiri mkubwa aliokuwa akiumiliki ulikuwa chini ya mke wake ambaye alimuacha akiwa na mtoto wake mdogo, Cynthia.
“Pole sana Anita! Mungu atakupigania tu,” alisema mama yake, bi Lydia.
“Nashukuru mama, asante kwa kunitia moyo katika kipindi hiki kigumu,” alisema Anita.
*****
Kitu kilichokuwa kikimuumiza Anita ni kumuona mpenzi wake wa kipindi cha nyuma, Edson akiwa kwenye hali ya umasikini mkubwa. Moyo wake uliumia mno, hakuamini kama kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akipata tabu kama alizokuwa akipata Edson.
Moyo wake ulimpenda mno, mbali na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa mwanaume huyo, pia alihitaji kuishi naye, yaani lile penzi la dhati alilokuwa nalo lirudi na kuwa kama zamani.
Anita hakutaka kutulia, ni mwezi mmoja tu ndiyo ulikuwa umepita tangu mazishi ya mumewe yalipofanyika lakini hakutaka kutulia, kila siku akawa mtu wa kumpigia simu Edson na kuzungumza naye, alishindwa kuzizuia hisia za kimapenzi alizokuwa nazo juu yake hivyo kumwambia ukweli.
Edson hakutaka kupinga, alijua hilo lingetokea na yeye mwenyewe alimpenda mno mwanamke huyo, hivyo kuanza kwenda kwake na kufanya mambo mengine kama wapenzi.
Kwenye kitanda kilekile alichokuwa akikitumia na mumewe ndicho hichohicho alicholala na Edson, hakutaka kujali sana kuhusu Phillip kwani kama kufa alikwishakufa hivyo asingeweza kurudi tena duniani.
Uhusiano huo uliendelea kwenda mbele, waliendelea kupendana kama zamani. Ndugu wa Phillip waliposikia kwamba Anita aliamua kuwa na mwanaume mwingine, mioyo yao iliumia sana, hawakuamini kwamba Anita hakusubiri hata miezi sita iishe, aliamua kuwa na mwanaume mwingine kwa haraka sana.
“Jamani! Nasikia Anita amepata mwanaume mwingine!” alisema ndugu mmoja huku akionekana kushangaa mno.
“Hata mimi mwenyewe Joshua aliniambia hivyohivyo, bado sijapata uhakika, hebu nikamuulize Joyce, anaweza akawa anajua,” alisema msichana mwingine.
“Lakini mbona amefanya haraka sana?”
“Hata mimi sijui kwa nini, unajua ni miezi miwili tu imepita.”
“Ndiyo hivyo! Ninachojiuliza, ni kwa muda gani alikutana na mwanaume huyo, kuzungumzia mapenzi mpaka kuwa wapenzi, ni muda mchache sana, yaani sijui nini kilitokea,” alisema msichana huyo.
Kila mmoja alishangaa, kila walichojiuliza, hawakupata jibu lolote lile. Mioyoni mwao waliumia lakini hawakuwa na jinsi, Anita aliamua kuwa na mwanaume mwingine hivyo hakutaka kuingiliwa.
Baba yake Edson aliposikia hivyo, hakutaka kukubali hata kidogo, alichokuwa akikiangalia ni mjukuu wake, Cynthia tu, alichokifanya ni kuwasiliana na Anita, majibu aliyopewa ni kwamba asiingiliwe, alichokiamua kilikuwa ni matakwa yake, hivyo hakutaka kuingiliwa.
“Unasemaje?”
“Ndivyo alivyoniambia! Tusimuingilie,” alisema baba Edson.
“Anita hawezi kubadilika namna hiyo! Kweli?”
“Ndiyo!”
“Hapana!”
“Kwani kwenye simu hujasikia mke wangu? Amenijibu tena kwa nyodo.”
“Yaani Anita huyuhuyu?”
“Ndiyo!”
Alichokifanya baba Edson ni kuwasiliana na wazazi wa Anita ambao wakamuita binti yao na kumwambia kwamba hakutakiwa kuwa na uhusiano na mwanaume yeyote yule mpaka kipindi cha miezi sita kipite.
MAjibu waliyopewa na binti yao, hayakuwa mazuri, bado msichana huyo hakutaka kuingiliwa katika maisha yake. Wazazi wake walihuzunishwa na majibu ya binti yao, walijaribu kumuomba kwamba auondoe moyo wake kwa Edson lakini msichana huyo hakukubali, kwa wakati huo, hakukuwa na mwanaume aliyeuteka moyo wake zaidi ya Edson.
“Tunataka uachane naye, mlee mwanao kwanza,” alisema baba yake.
“Jamani mbona tunaingiliana? Baba, ulivyoanza uhusiano na mama kuna mtu aliwaingilia?” alihoji Anita.
“Anita…maneno gani hayo?”
“Nimeuliza tu! Kama hakuna aliyewaingilia, kwa nini nyie mnaniingilia mimi?” aliuliza Anita.
Anita alibadilika, alionekana kuwa jeuri, hakutaka kusikia kitu chochote kile kutoka kwa mtu yeyote, alichokiangalia kwa wakati huo ni kuwa na Edson tu. Alimpenda zaidi ya mtu yeyote, katika maisha yake, hakukuwa na mtu ambaye angeweza kumtenganisha na Edson.
Miezi ikakatika, mwaka mwingine ukaingia, Cynthia akatimiza miaka mitatu hivyo kuanza kusoma shule ya chekechea katika Shule ya Kimataifa ya St. Augustine, shule iliyokusanya watoto wengi wa watu wenye hela.
Japokuwa maisha yalikuwa ya kifahari, alipata alichokitaka lakini Edson hakuonekana kuwa na furaha, kila siku alionekana kuwa na mawazo mengi, alionekana kama mgonjwa hali iliyomuweka Anita kwenye wakati mgumu.
ITAENDELEA KESHO

Facebook Comments

Tags
Show More

Related Articles

Close