Simulizi

NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU – 04

Miezi ikakatika, mwaka mwingine ukaingia, Cynthia akatimiza miaka mitatu hivyo kuanza kusoma shule ya chekechea katika Shule ya Kimataifa ya St. Augustine, shule iliyokusanya watoto wengi wa watu wenye hela.
Japokuwa maisha yalikuwa ya kifahari, alipata alichokitaka lakini Edson hakuonekana kuwa na furaha, kila siku alionekana kuwa na mawazo mengi, alionekana kama mgonjwa hali iliyomuweka Anita kwenye wakati mgumu.
Hakupenda kumuona mwanaume wake akiwa hivyo, kitendo cha kuonekana mnyonge hata yeye mwenyewe kilimshangaza mno. Aliumia moyoni, alijua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea ila Edson alifanya kuwa siri kubwa.
Kuvumilia kwake kukaisha, hakutaka kuendelea kujiuliza maswali mengi juu ya kilichomsibu Edson, alichokifanya Anita ni kumuita na kumuuliza kile kilichokuwa kikiendelea ambacho kilimfanya kuwa kwenye hali ile.
“Tatizo nini mpenzi?” aliuliza Anita.
“Hivi unanipenda kweli?” aliuliza Edson.
“Ndiyo! Ninakupenda mpenzi.”
“Kweli?”
“Hakika! Hakuna mwingine zaidi yako!”
“Haiwezekani! Sidhani kama ni kweli!”
“Kweli mpenzi! Ninakupenda. Unataka nikufanyie nini mpaka ujue kwamba ninakupenda?” aliuliza Anita.
Edson hakuzungumza kitu, akabaki kimya huku akiwa amejiinamia. Bado alijifanya kuwa na mawazo mengi, Anita alibaki akimwangalia huku akihisi moyo wake kuumia mno. Alichokifanya ni kumsogelea na kumuinua, alipomwangalia Edson, machozi yalikuwa yakimtoka mwanaume huyo.
“Unalia nini tena mpenzi?” aliuliza Anita.
“Kwa sababu haunipendi!”
“Ninakupenda mpenzi! Ninakupenda na ndiyo maana upo hapa!”
“Hapana Anita! Sidhani kama ni kweli!”
“Edson! Niambie mpenzi nikufanyie nini!”
“Mimi ni nani kwako?”
“Mpenzi wangu!”
“Na umesema kwamba muda si mrefu tutaoana, si ndiyo?”
“Ndiyo mpenzi!”
“Sasa mbona kila kitu unajimilikishia wewe tu?”
“Sijakuelewa.”
“Namaanisha mali. Yaani kila kitu unataka uonekane wewe tu.”
“Yaani bado sijakuelewa.”
“Namaanisha mbona na mimi hutaki kunipa haki yangu!”
“Ipi?”
“Ya kumiliki!”
“Hizi mali?”
“Ndiyo!”
“Sasa hilo ndiyo linakufanya uhuzunike hivyo?”
“Sasa unafikiri nitakuwa na furaha? Naendesha magari ya kifahari, ila sina haki nayo, naishi kwenye nyumba nzuri, ila sina haki nayo, nasimamia mpaka biashara ambazo sina haki nazo. Sasa haki zangu zipo wapi?” alihoji Edson.
“Sasa ndiyo ukasirike na kuonekana kama mgonjwa?”
“Ndiyo hivyo!’
“Basi usijali mpenzi, nitakuandikisha na wewe uwe na haki nazo,” alisema Anita maneno yaliyomfanya Edson kuwa na furaha mno.
Hilo ndilo alilolitaka, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali kila alipojiona akiendesha magari ambayo si yake au kuishi ndani ya nyumba ambayo haikuwa na haki yake. Kila siku katika maisha yake alitamani naye awe na asilimia fulani katika kumiliki mali zile alizokuwa nazo Anita.
Kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo Anita kwa Edson, akajikuta akimuita mwanasheria wake na hatimaye kumuandikisha Edson kuwa mmiliki halali kama alivyokuwa.
Kwa Edson, hiyo ilikuwa furaha kubwa, hakuamini kama kila kitu kingekwenda kwa wepesi kama kilivyokuwa. Akajikuta akimkumbatia Anita na kummwagia mabusu mfululizo, hapo, akamwambia kwamba moyoni mwake alikuwa na amani, furaha aliyokuwa nayo haikuelezeka.
Anita alimpenda sana Edson lakini mwanaume huyo, moyoni mwake alikuwa akifikiria kitu kingine kabisa, hakujiona kama alikuwa na mapenzi makubwa kwa msichana huyo kama kipindi cha nyuma, kitu ambacho kilimfanya kujifanya kuwa na mapenzi mazito kwa msichana huyo ni mali alizokuwa nazo tu.
Alizitamani mali zile, alitaka sana ziwe zake, hivyo kitendo cha kuandikishwa kama mmiliki halali wa zile mali, moyoni mwake ilikuwa ni shangwe kubwa.
Akapanga mipango yake, kitu pekee alichotaka kufanya ni dhuluma tu, alitaka kumdhulumu mwanamke huyo mali zile, ziwe zake na kufanya mambo yake, azitumie atakavyo.
“Ameingia kingi! Ataisoma namba sasa,” alisema Edson huku meno yote yakiwa nje.
****
Siku zikaendelea kukatika, baada ya miaka miwili kupita huku Cynthia akiwa na miaka mitano, hapo ndipo Edson alipoanza kubadilika. Akaanza dharau kwa Anita, kila alipoambiwa hili na lile, alibadilika na hakutaka kusikia hata mara moja.
Akawa mtu wa kunywa pombe, kurudi usiku wa manane na hata wakati mwingine kuwaingiza wanawake ndani ya nyumba hiyo kitu kilichomuuma sana Anita.
Hakuwa na msemo wowote ule. Kwa kipindi kirefu alimwambia kwamba ilikuwa ni lazima waoane lakini kwa kipindi hicho, Edson hakutaka kusikia chochote kile, hakutaka kusikia mambo ya ndoa kwani kile alichokitaka alikifanikisha kwa kiasi kikubwa.
Alitaka kila kitu kiwe chake, hivyo akaanza kuhamisha fedha zilizokuwa kwenye akaunti za Anita na kuziingiza katika akaunti yake. Kiasi cha shilingi bilioni sitini kikaamishwa na kuingizwa katika akaunti yake.
Anita hakufahamu kilichokuwa kikiendelea, kila kitu alichangia na Edson, hakujua kama mule ndani ya akaunti yake ni milioni kumi tu ndizo zilizokuwa zimebaki.
Maisha yalibadilika, hayakuwa yale yenye mapenzi kama yalivyokuwa kipindi cha nyuma, Edson yule alibadilika, Anita hakuamini kama mwanaume yuleyule aliyemkuta akiwa amechoka katika kampuni moja ya boti za Royal Palm ndiye ambaye leo hii alikuwa akimfanyia mambo yale.
Moyoni aliumia, wakati mwingine alijuta sababu ya kumwandika kama mmoja wa wamiliki wa mali zile.
Hapo ndipo tabia halisi ya Edson ilipoanza kuonekana, ulevi ukamteka, mara kwa mara akawa mtu wa kurudi usiku wa manane. Kila Edson anapokuwa nje, Anita hakulala, alibaki macho huku akimsubiria mwanaume huyo.
Mateso aliyoyapata yalikuwa siri, hakutaka kumwambia mtu yeyote kwa kuogopa kuchekwa na kudharauliwa. Alikuwa mtu wa kujifungia chumbani, wakati mwingine alibaki akilia tu, kila kilichokuwa kikiendelea, hakika kilimuumiza mno.
“Edson…mbona umebadilika hivi?” aliuliza Anita.
“Nani? Mimi?”
“Ndiyo! Haukuwa hivi zamani, nini kimekubadilisha?” aliuliza Anita, machozi yalianza kumlenga.
“Hebu niondolee uchuro wako huko,” alisema Edson huku chupa ya Saint Anna ikiwa mkononi mwake.
Kubadilika kwa Edson kuliendelea kumshangaza sana Anita, hakutaka kukubali, alijua kulikuwa na kitu kilichomfanya kuwa hivyo, akili yake ikamwambia kwamba ilikuwa ni lazima afuatilie suala la fedha katika akaunti zake kwa kuhisi kwamba Edson angeweza kumtapeli.
Hapo ndipo alipoanza kufuatilia, alipokwenda kwenye akaunti ya kwanza, hakukuta kiasi cha fedha kikubwa, ni milioni tano tu ndizo zilizokuwa zimebaki.
Alishtuka mno, hakuamini macho yake, hakutaka kuishia hapo, alipoangalia akaunti ya pili, pia kulikuwa na shilingi milioni tano tu. Alijikuta miguu yake ikiisha nguvu, ikalegea na hapohapo kuanza kulia kama mtoto.
“Kuna nini dada?” aliuliza mfanyakazi wa benki, si yeye aliyeshangazwa na kilio cha Anita, hata wafanyakazi wengine na wateja waliokuwa humo ndani walishangazwa naye.
Watu wakaanza kumbembeleza Anita, walimtaka anyamaze lakini pia walitaka kufahamu tatizo lilikuwa nini. Anita hakunyamaza, kilichokuwa kimetokea, wakati mwingine alihisi kama yupo ndotoni na baada ya muda mchache angeamka kutoka usingizini.
Anita hakutaka kubaki hapo benki, alichokifanya ni kuondoka huku akiwa amechanganyikiwa, alipofika nje, akalifuata gari lake la thamani na kuingia, safari iliyoanza ni kwenda nyumbani kwake.
Aliendesha gari huku akiwa amechanganyikiwa, kila aliposogea mbele, alisikia maumivu mazito moyoni mwake. Hakuamini kama Edson yuleyule ndiye aliyefanya vile, hakuamini kama shukrani ya punda aliamua kumpiga mateke.
Kwa kuwa hakukuwa na foleni, hakuchukua muda mrefu akawa amekwishafika nyumbani, geti likafunguliwa na kuingia ndani.
“Hili gari la nani?” aliuliza Anita mara baada ya kuingia ndani ya eneo la nyumba yake.
“Kuna wageni wamekuja.”
“Wakina nani?”
“Sijui! Ila shemeji amesema ni wateja wamekuja kununua nyumba.”
“Nyumba ipi?”
“Hiihii!”
Anita alihisi kuchanganyikiwa zaidi, hakuamini kile alichokisikia kwamba kuna wageni wamekuja kwa lengo la kununua nyumba. Akaingia ndani mpaka sebuleni, macho yake yakagongana na wanaume wawili waliovalia suti ambao walikaa kwa kujiachia sebuleni pale.
Mbali na wanaume hao, pia Edson alikuwa sebuleni hapo akiwa amejiachia tu, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.
“Milioni mia moja na hamsini,” alisema Edson, alijifanya kama kutokumuona Anita.
“Basi hakuna tatizo! Hati iko wapi?”
“Hilo halina tatizo!”
“Sawa! Kesho nitakuandikia cheki,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa kijana tu.
Anita hakuamini alichokisikia, mapigo ya moyo wake yalidunda kwa nguvu, hakuamini kile alichokiona, hakuamini kama hao waliofika nyumbani hapo walikuwa wateja waliotaka kununua nyumba pasipo yeye kushirikishwa.
Moyo wake ulikuwa na hasira mno, alitoka benki ambapo huko alikuta kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimechukuliwa, wakati akirudi nyumbani huku akionekana kuwa na hasira, akakutana na kitu kingine kabisa, wageni walifika mahali hapo kwa ajili ya kununua nyumba yake.
“Edson! Unataka kuiuza nyumba yangu?” aliuliza Anita huku akionekana kutokuamini.
“Kuuza nyumba yako au yetu?”
“Yetu! Tangu lini? Umechangia hata tofali humu?” aliuliza Anita, hakuamini kama siku hiyo alimfokea Edson.
“Kwani hati ya nyumba inaonyesha ni nani mmiliki halali wa nyumba hii?”
“Mimi?”
“Umenisahau hata mimi? Sikiliza Anita, mimi kama mmoja wa wamiliki wa nyumba hii, nimeamua kuiuza kwa kuwa nimechoka kuishi humu, ni bora nyumba iuzwe, tugawane pesa halafu kila mtu afanye yake,” alisema Edson.
Anita alibaki akibubujikwa na machozi tu, hakuamini kama kile kilichokuwa kikitokea. Aliachiwa mali na mumewe, aliachiwa fedha nyingi lakini mwisho wa siku, kila kitu kilikuwa kikiporwa na mwanaume aliyeonekana kuwa katili.
Hakuacha kulia, aliumia mno lakini machozi yake yote, hasira zake zote hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile, ukweli ulibaki palepale kwamba nyumba ilitakiwa kuuzwa na kisha agawane hela na Edson, mtu ambaye hakuwahi hata kutokwa jasho kuzitafuta.
Baada ya wiki moja, uuzaji wa nyumba ile ukakamilika, haikuwa mali yake tena, ilikuwa mali ya mtu mwingine, mmiliki mpya aliyejulikana kwa jina la Andrew Nkone.
Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Anita, bado hakuamini kilichokuwa kimetokea kwamba alipoteza nyumba na kiasi kikubwa cha fedha. Hakukuwa na sehemu ya kukimbilia, kila alipokwenda, hakupata msaada wowote ule mpaka pale alipoashauriwa kwamba ilikuwa ni lazima kesi hiyo ifikishwe mahakamani ili aweze kushinda haki yake.
“Itawezekana kweli?”
“Kwa nini isiwezekane?”
“Naona inaweza kuwa na ugumu.”
“Hakuna kitu kama hicho! Wewe nenda tu.”
Alichokifanya ni kuonana na mwanasheria wake na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea hivyo kesi kufunguliwa na kuanza kusikilizwa mahakamani.
“Hii ni kesi ya madai, nina uhakika utafanikiwa tu, utashinda na kila kitu kurudi kwako,” alisema mwanasheria wake aitwaye Sifaeli Mambo.
“Nitashukuru sana, naomba unisaidie.”
“Hilo wala usijali.”
Kilichotokea ni Edson kuitwa mahakamani na kusomewa kesi ya madai iliyokuwa imepelekwa katika mahakama hiyo huku mshtaki akiwa Anita. Edson hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule, kila kitu kilichokuwa kimetokea, alikuwa na uhakika kwamba angeshinda kesi ile na hivyo kujimilikisha haki za umilikaji wa mali na fedha zile moja kwa moja.
Wakati kesi ikiunguruma mahakamani, hakukuwa na ndugu yeyote wa Anita au marehemu mume wake aliyekwenda mahakamani, walitokea kumchukia Anita kutokana na kile alichokuwa amekifanya hivyo nao walimwachia afuatilie kila kitu peke yake.
Mtu ambaye alikuwa tumaini lake kwa wakati huo alikuwa mtoto wake tu ambaye katika kipindi hicho alikuwa na miaka sita. Kila siku Cynthia alionekana kuwa na huzuni mno, kila alipomuona mama yake akilia, moyo wake ulimuuma sana, hakujua mama yake alilia nini, alijitahidi kuuliza lakini Anita hakutaka kumwambia ukweli, alimficha.
Tofauti na kesi nyingine, kesi hiyo ilisikilizwa kwa muda wa miezi miwili tu tena huku ikisimamiwa na hakimu aliyejulikana kwa jina la James Marimba. Hukumu ya kesi ile ilivyotoka ilionyesha kwamba Anita alipoteza haki zake za kumiliki mali zote, si hizo tu na hata fedha ambazo alitakiwa kuzimiliki, hakuwa na haki nazo.
Kilisikika kilio kikubwa mahakamani hapo, hakuamini kama hakimu ndiye aliyetoa hukumu hiyo nzito. Alipoteza kila kitu, alimpenda Edson, alimthamini na kumpa kila kitu alichokihitaji kikiwepo uhalali wa kumiliki mali lakini mwisho wa siku ni maumivu makali ndiyo yaliyofuata.
Akaachwa yeye kama yeye, hakuwa na fedha, hakuwa na mahali pa kuishi, akajaribu kwenda kwa ndugu zake, wote aliowafuata, hakukuwa na aliyetaka kuishi naye, wengi walimfukuza.
Huku akiwa na mtoto wake, hakuwa na jinsi, akaondoka na kwenda mitaani. Huko, akaanza kuishi maisha ya mitaani, hakukuwa na aliyeamini kwamba mwanamke yule aliyekuwa na utajiri mkubwa hatimaye ndani ya miaka mitatu tu, alikuwa masikini wa kutupwa, aliyelala mitaani huku akiwa na binti yake mdogo.
Aliogopa kwenda nyumbani kwao, alikumbuka namna wazazi wake walipomuita na kumwambia kuhusu Edson, walimkataza kuwa na mwanaume huyo hivyo abaki peke yake na kumlea mtoto wake lakini majibu yaliyotoka kinywani mwake, yalionyesha dharau ya hali ya juu.
Leo hii, hakutaka hata kwenda huko nyumbani, moyo wake ulimuhukumu, hakuwa na furaha, alijiona kutengwa na dunia nzima, kulia ikawa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
Kwa sababu hawakuwa na fedha, waliingia kwenye umasikini mkubwa, Cynthia akafukuzwa shule ya kimataifa aliyokuwa akisoma ambayo kwa mwaka ada yake ilikuwa ni zaidi ya milioni mbili.
Wakati akiendelea kuteseka mitaani ndipo alipofuatwa na watu wawili na kupewa taarifa kwamba alikuwa akihitajika na wazazi wake, walimsamehe kwa kila kitu kilichotokea na hivyo walihitaji kuishi naye.
Kidogo kwake ikaonekana kuwa nafuu, akaelekea nyumbani kwa wazazi wake ambapo baada ya kuwaona tu, akaanza kuwaomba msamaha kwa yote yaliyotokea.
“Usijali binti yetu, tumekusamehe,” alisema baba yake.
Nyumbani kwao hakukuwa na maisha mazuri, kipindi cha nyuma alikuwa akiwasaidia sana wazazi wake lakini baada ya mali kuzikabidhi kwa Edson, kila kitu kikabadilika, misaada haikwenda tena kwa wazi wake, fedha zile zilizokuwa kwenye akaunti zikawekewa mipaka, na kwa sababu alimpenda sana Edson, hakutaka kujali sana kwani mapenzi yalimlevya.
Leo hii, aliona ubaya wa Edson, alijuta kwa kutokuwasikiliza wazazi wake.Mapenzi yalisababisha kila kitu kilichotokea, mapenzi yakasababisha kupoteza kila kitu alichokuwa nacho.
Kulia hakukusiha, hata kula hakula, moyo wake ulimuuma sana. Mara kwa mara aliwasiliana na wakili wake na kumuuliza namna kesi ile waliyoshindwa.
Kwa jinsi ilivyoonekana tu, ilionyesha kuwa kulikuwa na mazingira ya rushwa yaliyohusika na ndiyo maana ilikuwa nyepesi mno kwa Edson na ngumu mno kwake.
Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Wakati mwingine alikaa na kumlaumu Mungu sababu ya kumchukua mume wake mapema mno hata kabla binti yake hajawa mkubwa.
“Mungu! Kwa nini mimi? Kwa nini Edson amenidhulumu mali zangu?’ aliuliza Anita huku akilia.
Pamoja na machozi yote, pamoja na huzuni zote, majonzi lakini ukweli ulibaki palepale kwamba alidhulumiwa mali zake na mwanaume aliyekuwa akimpenda ambaye aliamini kwamba angesaidiana naye kuzikuza mali zile.
*****
Kila kitu kilikamilika, kwenye suala la fedha, Edson alionekana kuwa makini mno, alitaka kumtumia rafiki yake ambaye alikuwa na fedha nyingi, Nkone kwa ajili ya kuhakikisha kwamba nyumba ile inakuwa yake.
Kazi kubwa ya Nkone ilikuwa ni kujifanya mnunuzi wa nyumba ile, kwamba mara Anita atakapoulizia mnunuzi basi Nkone ajitokeze na kusema kwamba yeye ndiye mnunuzi lakini ukweli ulibaki palepale kwamba mwanaume huyo hakuinunua nyumba ile bali ilikuwa mikononi mwa Edson.
Walifanikiwa kufanya mchezo huo mchafu, Anita akadhulumiwa nyumba yake na hivyo kwenda kuishi na wazazi wake. Edson na Nkone walibaki wakipongezana kwa kazi kubwa waliyokuwa wameifanya.
Baada ya kuona kwamba Anita alitaka kuipeleka kesi mahakamani, walichokifanya ni kuzungumza na hakimu James Marimba na kumwambia jinsi hali ilivyokuwa na kwamba kama angefanikisha kushinda kwa kesi ile basi kitita cha shilingi milioni mia mbili kilikuwa mezani.
Kilikuwa ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angekikataa, alichokifanya ni kukubaliana nao na ndiyo maana kesi ikapelekwapelekwa tu na mwisho wa siku Edson kushinda katika mazingira ya kutatanisha sana.
Baada ya kufanya michezo hiyo michafu ndipo walipoamua kukutana na kusherehekea, kwao ulionekana kuwa ushindi mkubwa. Wakaitana kwenye Hoteli ya New Paradise ambapo huko, wakala na kunnywa na baada ya hapo Edson kuingizwa katika idadi ya mabilionea wakubwa nchini Tanzania.
“Karibu katika ulimwengu wa mabilionea,” alisema Nkone.
“Asante sana, cha msingi ni kuziongeza fedha hizi ziwe nyingi zaidi, nitataka kufungua biashara nyingi,” alisema Edson.
“Hilo ni la maana sana. Nitakuwa pamoja nawe, nitakuonyeshea michongo mingi ya biashara,” alisema Nkone.
ITAENDELEA KESHO

Facebook Comments

Tags
Show More

Related Articles

Close