Simulizi

Niliua Kumlinda Mama Yangu – 05

“Karibu katika ulimwengu wa mabilionea,” alisema Nkone.
“Asante sana, cha msingi ni kuziongeza fedha hizi ziwe nyingi zaidi, nitataka kufungua biashara nyingi,” alisema Edson.
“Hilo ni la maana sana. Nitakuwa pamoja nawe, nitakuonyeshea michongo mingi ya biashara,” alisema Nkone.
Hicho ndicho kilichofuata, Edson akajiingiza katika biashara za kuuza magari ambazo kwa namna moja au nyingine zikamfanya kuwa tajiri mkubwa. Kila siku aliogelea katika bwawa la fedha, hakumkumbuka kabisa Anita, wakati mwingine aliona kwamba msichana huyo na mume wake waliandaliwa kwa ajili yake, yaani wapate utajiri ambao baadaye ungekuja na kuwa wake.
Jina lake likaanza kuwa kubwa, wanawake wakaanza kumpapatikia, kila alipopita, watu walimzungumzia yeye kwa kuwa tu alikuwa na utajiri mkubwa ambao hakukuwa na mtu aliyejua kwamba utajiri wote huo alikuwa amemdhulumu Anita.
Wanawake wa mjini waliojua namna ya kuzitafuna pesa za wanaume hawakumuacha Edson, kila siku walijilengesha kwake, walijiweka katika mikao iliyojaa mitego ambayo ilimfanya mwanaume huyo kuingia kwenye kumi na nane zao, kilichofuata ni kuponda raha naye.
Katika wanawake wote aliokuwa akiponda nao raha, alikuwepo mmoja ambaye alimshikilia hasa, huyu aliitwa Jamila. Alikuwa msichana mrembo wa sura, mweupe, mwembamba lakini huko nyuma ndiyo ilikuwa balaa.
Kila alipotembea, kulitingishika, kwenda kulia na kushoto. Siku ya kwanza Edson alipomuona Jamila, alishtuka, hakuamini kama angeweza kumuona msichana kama huyo jijini Dar es Salaam kwani aliamini wanawake wengi wa namna hiyo walipatikana Mombasa.
Akashindwa kuvumilia, siku ya kwanza alipopewa penzi, likamchanganya, hakutaka kusikia chochote kile, yeye na Jamila wakawa kama mama na mwana, kila walipokwenda, walikuwa pamoja, waliyafaidi mapenzi huku Edson akipewa kila alichokitaka kutoka mwilini mwa Jamila.
“Baby! Nataka wiki ijayo tusafiri!” alisema Jamila.
“Kwenda wapi?”
“Popote penye baridi kidogo, Tanzania joto sana.”
“Basi twende Uingereza au Hispania, unaonaje?”
“Hakuna tatizo! Tutakwenda huko.”
Maisha yalihitaji nini tena? Hakuwa na shida kama kipindi cha nyuma, kwa wakati huo Edson alikuwa akinukia pesa, hakukumbuka kama miezi michache iliyopita alikuwa katika maisha ya ufukara yaliyomfanya kurandaranda mitaani kutafuta chakula tu.
Baada ya miezi miwili, akapata taarifa kwamba yule hakimu ambaye alisimamia kesi yake, bwana James Marimba aliachana na kazi hiyo na hivyo kujiingiza kwenye biashara.
Hapo ndipo walipoanza kujenga urafiki mkubwa. Yeye na bwana Nkone wakamchukua Marimba na kumuingiza katika system yao na hivyo kuanza kushirikiana katika biashara zao.
Wao watatu wakatengeneza mtandao mkubwa, wakapanua biashara zao na hivyo kuingiza kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti zao. Maisha yalibadilika, wakajikuta wakianza kujulikana nchini Tanzania, wakatengeneza majina yao kwa kuwatumia vijana.
Walijua kwamba vijana walikuwa na nguvu kubwa hivyo wakawashikilia vilivyo. Wakaanza kuwapatia fedha, kuwasaidia katika kununua pikipiki za kufanyia biashara, hiyo yote ni kwa sababu walitaka kujitangaza na kujulikana nchini Tanzania.
Walitaka kuonekana kama watu wema, wawasaidie vijana wengi lakini upande wa pili walikuwa na mpango kabambe wa kufanya biashara za magendo, kuuza madawa ya kulevya na kuua tembo katika mbuga mbalimbali za wanyama.
Walifanikiwa katika mipango yao, vijana waliwatangaza, wakaonekana kuwa watu bora, matajiri wasiokuwa na sifa ambao kila siku walitamani watu wengine kupata hata robo ya kile walichokuwa nacho.
Ili kuwafanya watu kutokuingilia mambo yao ya biashara za magendo ambayo walitaka kufanya, kwanza wakajiweka karibu na jamii, yaani kwa Nkone, kitu alichokifanya ni kuisaidia jamii kwa kuwaletea chakula kutoka mikoani.
Alipokwenda Mbeya, alinunua mpunga kwa bei waliyoitaka wakulima, hakujali kama ilikuwa kubwa au la, alipohakikisha manunuzi yamefanyika, alisafiri mpaka Dar es Salaam huku akiwa na tani zaidi ya mia moja na kuelekea masokoni, huko, mchele aligawa bure kabisa kwa kila mtu aliyetaka.
Ilikuwa ni kazi ya kujitoa ambayo ilimfanya kupoteza kiasi kikubwa cha fedha, yeye, hakuangalia hicho, alichokitaka ni kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa kama kilivyotakiwa kuwa.
Watu wakawapenda, hakuishia kwenye mpunga tu, bali ngano, unga na vitu vingine vyote alivipeleka jijini Dar es Salaam na kuwasaidia watu mbalimbali waliofika jijini humo na hata wale waliotoka mikoani.
Jina la bwana Nkone likawa kubwa, akajulikana sana kiasi kwamba kila alipopita, watu walikuwa tayari kulisimamisha gari lake, kulisafisha kisha kumwambia aendelee na safari na huku wakati mwingine wakidiriki mpaka kupiga deki barabara.
“Huyu jamaa atakuwa malaika tu,” alisema kijana mmoja.
“Kwa nini?”
“Haiwezekani kuwe na binadamu mwenye roho nzuri kama hii. Jamaa anatoa chakula kutoka mikoani na kuja kugawa bure, hivi kuna mtu anaweza kuwa na moyo huo?” alihoji kijana huyo.
Ukiachana na huyo, mtu mwingine, bilionea ambaye aliibuka alikuwa bwana Marimba. Huyu naye alikuwa na moyo wa kuwasaidia Watanzania, alitaka watu wote waliokuwa na magonjwa ya moyo wapate tiba bure kabisa na kusiwepo na wagonjwa wa kusafiri kwenda India kutafuta tiba.
Akajenga hospitali kubwa jijini Dar ambayo iliwashughulikia zaidi wagonjwa wa magonjwa ya moyo. Kwake, hiyo ilikuwa sifa kubwa, watu wengi walimsifia kwamba alikuwa na moyo mzuri kama bwana Nkone.
Hakuishia hapo, alichokifanya ni kupanga mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana bure kabisa kwenye hospitali zote, gharama zilikuwa chini yake.
Alipoteza kiasi kikubwa cha fedha lakini hakuangalia, alichokitaka ni kujenga uaminifu katika jamii kwani kile alichotaka kukifanya na mabilionea wenzake kilikuwa kikubwa mno ambacho kingewaingizia fedha kupita kawaida.
“Gharama za dawa kiasi gani?” aliuliza mgonjwa mmoja katika hospitali moja jiji Dar es Salaam, alionekana kuwa hoi.
“Zote ni elfu themanini!”
“Mmh! Jamani dokta, nitaweza kulipia kweli na maisha yangu magumu?”
“Usijali! Umekwishalipiwa.”
“Nimelipiwa! Na nani?”
“Na bwana Nkone. Analipia gharama za dawa zote,” alisema daktari.
Kama ilivyokuwa kwa Nkone hata kwake alijijengea heshima kubwa, Watanzania wakachanganyikiwa, mapenzi waliyokuwa nayo juu yake yalikuwa makubwa mno, hawakuamini kama kungetokea mtu ambaye angekuwa tayari kuingia gharama kwa ajili ya Watanzania.
Wagonjwa wa magonjwa ya moyo wakafika katika hospitali yake, huko, walipatiwa matibabu bure tena kutoka kwa madaktari waliobobea katika magonjwa hayo.
Ilikuwa sifa kwa Watanzania kwani pia wagonjwa wengi kutoka Rwanda, Kenya na Uganda walifika Tanzania kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Edson ambaye baada ya kupata ubilionea aliamua kuitwa jina lake la pili la Kambani kama ubini wake, akaamua kuwasaidia Watanzania katika kujenga viwanda vya makaratasi, viatu na nguo na kuwaajiri Watanzania wengi tena wa rika zote.
Alipoona amefanikisha katika hilo, akaanza kujenga vituo vya watoto yatima, watoto wote waliokuwa wakizurura mitaani wakachukuliwa na kupelekwa katika vituo hivyo ambapo huko walisomeshwa, walilishwa na kuvarishwa kama watu wengine.
Kambani hakuishia hapo, alichokifanya ambacho kikaonekana kuwa kama kujitangaza zaidi ni kusaidia kujenga misikiti na makanisa. Kupitia msaada huo, akajikuta akipata jina kubwa zaidi nchini Tanzania.
Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliosema maneno mbalimbali lakini hakuacha, misikini na makanisa ambayo ilisimamisha ujenzi kwa kuwa watu walikosa fedha, aliimalizia na maisha kuendelea.
Akajijengea jina kubwa, utajiri wake ukaongezeka, kila alipopita, watu walimpongeza, walimsifia kitu kilichomfanya yeye na mabilionea wengine kuitwa sana ikulu.
Huko, walipongezwa kwa kazi kubwa waliyoifanya pasipo Watanzania kujua kwamba mbali na misaada hiyo, watu hao walikuwa na mawazo ya kujiingiza katika biashara haramu za kuuza madawa ya kulevya na kuua wanyama mbugani ili kuongeza utajiri wao. Hilo, Watanzania hawakulifahamu.
*****
Miaka mitano ikapita, utajiri wao ulikuwa mkubwa zaidi, ile mipango waliyokuwa wameiweka, ikafanikiwa na katika kipindi hicho walikuwa wakiingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia madawa ya kulevya na kuua wanyama wengi mbugani.
Hakukuwa na mtu aliyefahamu kama yale madawa ya kulevya ambayo yaliingizwa sana nchini yalikuwa chini yao. Kwa viongozi ambao walijua, walinyamazishwa kwa kupewa kiasi fulani cha fedha, hivyo wakanyamaza.
Mara kwa mara waliwatuma vijana wao kwenda Pakistan ambapo huko walichukua madawa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na kuyaleta nchini Tanzania ambapo yaliuzwa hapo na mengine kupelekwa sehemu mbalimbali barani Afrika.
Wao ndiyo walikuwa wasambazaji wakubwa wa madawa ya kulevya barani Afrika. Kila mzigo uliokuwa ukiingia Afrika ilikuwa ni lazima upite mikononi mwao na kuwatuma vijana kusambaza katika nchi mbalimbali.
Wakawa na genge la watu zaidi ya ishirini, tena vijana wa kike na wa kiume ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kusambaza madawa hayo sehemu mbalimbali.
Ilikuwa ngumu mno kuwagundua, misaada waliyoitoa kwa jamii iliwafanya watu kutokuamini hata pale tetesi za chini ziliposikika kwamba watu hao walijihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya.
Kwa kuwaangalia, walionekana kuwa wapole sana ambao waliwapenda watu wote pasipo kujua kwamba upande wa nyuma watu hao walikuwa wauaji wakubwa ambao kamwe hawakutaka kupata hasara.
Kila mtu aliyefika mbele yao na kusema kwamba mizigo ilikamatwa, aliuawa kwani katika biashara yao hiyo hawakutaka kupata hasara ya aina yoyote ile.
“Nisikilize Ali, unazingua…” alisema Kambani huku akionekana kuwa na hasira, mkononi mwake alikuwa na bastola.
“Nisamehe bosi, ilikuwa bahati mbaya.”
“Huo ni uzembe na lazima uulipe, yaani tupoteze bilioni moja kwa ajili yako, haiwezekani Ali ni lazima ufe,” alisema Kambani huku akiichukua bastola yake kutoka kiunoni.
“Bosi subiri kwanza.”
“Nisubiri nini? Hivi unafikiri tunafanya kazi ya kanisa? Hivi unafikiri hizi fedha tuliziokoka tu sehemu?” aliuliza Kambani.
“Bosi…bosi….”
“Paaa…paaaa…”
Ilisikika milio ya bastola ndani ya jumba hilo la kifahari, hapohapo, kijana yule aliyeitwa kwa jina la Ali akaanguka chini na damu kuanza kumtoka. Tofauti na mabilionea wengine waliokusanyika mahali hapo, Kambani alionekana kuwa na hasira mno, alijua kwamba alitoka kwenye maisha ya shida, yaliyojaa umasikini ambayo hakutaka kurudi tena, hivyo alitaka kuhakikisha anafanya lolote lile lakini mwisho wa siku utajiri wake kuendelea kuwepo.
Miaka mitano ilipita tangu aachane na Anita, hakutaka kumkumbuka kabisa, ule utajiri aliomdhulumu, alitaka kuuendeleza na kuwa bilionea mkubwa barani Afrika, hivyo ilikuwa ni lazima kuwamaliza vijana ambao walileta masihara.
“Nkone, hawa vijana wapumbavu sana, ukiwachekea, mwisho wa siku utajikuta unaendesha mkokoteni Tandale,” alisema Kambani huku akimwangalia Nkone.
“Kweli kabisa, ila ungempa nafasi nyingine.”
“Hakuna cha nafasi! Unafikiri amekamatwa kweli? Alitaka kutuchezea dili tu. Marimba, tunatakiwa tuwe makini sana. Umeachana na uhakimu ili utengeneze pesa, sasa wapumbavu kama hawa wakitokea, si utarudi tena kuwa hakimu na kula rushwa za shilingi elfu kumikumi? Tusitake masihara kabisa na pesa,” alisema Kambani.
Biashara zao za madawa ya kulevya zilizidi kusambaa, walizidi kupata wateja wengi barani Afrika, wakagawana majukumu kwamba ilikuwa ni lazima wahakikishe wanapata matawi zaidi, hivyo walichokifanya ni kuwafuata wasanii wa muziki na watu wengine maarufu na kuwatumia katika usambazaji wa madawa yao.
Ukiachana na hayo, pia walihakikisha wanacheza michezo michafu katika viwanja vya ndege, wakawakamata polisi wote ili kila mtu wao anapopita asiweze kupekuliwa, na hilo likafanyika kwa haraka sana.
Hakukuwa na uwanja wa ndege barani Afrika uliokuwa hatari kwao, kila uwanja walihakikisha wanaukamata vilivyo. Waliingiza fedha, walitanua kwa kununua magari ya kifahari ila pamoja na yote hayo, walihakikisha kwamba jukumu lao la kuisaidia jamii lilikuwa palepale na ndiyo kitu pekee ambacho kiliifanya hata serikali kutokuwafuatilia sana.
“Ni lazima tuishi kwa akili Kambani! Vipi kuhusu wale Waarabu?” aliuliza Nkone.
“Waarabu gani?”
“Wale wa Tunisia!”
ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA

Facebook Comments

Tags
Show More

Related Articles

Close