Simulizi

Niliua Kumlinda Mama Yangu – 06

“Ni lazima tuishi kwa akili Kambani! Vipi kuhusu wale Waarabu?” aliuliza Nkone.
“Waarabu gani?”
“Wale wa Tunisia!”
“Wako poa, leo asubuhi walinitaarifu kwamba mizigo imeingia bila matatizo na fedha watatuma jioni,” alisema Kambani.
“Safi sana!”
“Ila kuna kitu,” aliingilia Marimba.
“Kitu gani?”
“Unamkumbuka yule malaya uliyekuwa ukiishi naye?”
“Nimeishi na wengi! Yupi?”
“Yule mwenye mali.”
“Unamaanisha Anita?”
“Ndiyo!”
“Amefanya nini?”
“Unafikiri huu ndiyo utakuwa mwisho?”
“Kivipi?”
“Nina uhakika kuna siku atalianzisha tu! Yaani ile kesi inaweza kufufuliwa upya na akaja kushinda,” alisema Marimba.
“Ila wewe si ndiye uliimaliza mahakamani?”
“Ndiyo! Ila nimekumbuka kwamba nilifanya kosa!”
“Kosa lipi?”
“Nilipomaliza kesi ile nilisema kwamba mahakama ilikuona hauna hatia,” alisema Kambani.
“Si ndiyo sikuwa na hatia!”
“Ndiyo! Ila kuna kitu ambacho ni lazima ukifahamu.”
“Kipi?”
“Kuna utofauti kati ya mahakama kutokukuona kuwa na hatia na mahakama kukuachia huru,” alisema Kambani.
“Utofauti wake ni upi?”
“Mahakama inapokuona hauna hatia, inamaanisha kwamba jalada linafungwa na hivyo kesi kuisha ila mahakama inapokuachia huru, inamaanisha kwamba inawezekana kuna vipengele fulani havipo ila vipengele hivyo vikipatikana, kesi inaweza kuanza tena,” alisema Kambani.
“Sasa nani ataianzisha?”
“Kama huyo Anita akienda mahakamani, ni lazima jalada lifunguliwe tena, kesi ianze kuunguruma.”
“Daah! Kwa hiyo?”
“Tumuue huyu Anita kupoteza ushahidi! Vinginevyo, baadaye itakula kwako,” alishauri Marimba.
“Hakuna tatizo! Nipo tayari kuua ili kuzilinda mali zangu! Nipo tayari kumuua Anita.”
“Basi fanya hivyo! Anapoishi si unapajua?”
“Ndiyo!”
“Basi tuma vijana wakammalize.”
“Haina tatizo! Nitafanya hivyo leo hiihii,” alisema Edson Kambani na kuchukua simu yake, akawaambia vijana wake kwamba wafanye lolote liwezekanalo ili Anita aweze kuuawa haraka iwezekanavyo!
Alichokifanya ni kuwaambia mahali alipokuwa akiishi. Vijana hao wakasema kwamba ni lazima wafanye kazi hiyo. Hivyo wakajiandaa.
****
Binti yake alikuwa na miaka mitano tu, maisha yalimpiga mno mpaka yule Anita aliyeishi kitajiri kupigika, mwili kuchoka sababu ya mawazo mengi huku mara kwa mara akiumwa magonjwa mbalimbali, hiyo ilitokana na mawazo lukuki aliyokuwa nayo.
Bado moyo wake haukuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia maisha yale, kwake, hiyo ilionekana kuwa kama ndoto ambapo baada ya muda fulani angeshtuka na kujikuta kitandani, akiwa na mume wake mpendwa huku pembeni yake akiwepo binti yake aliyekuwa akimpenda mno.
Moyo wake ulimchukia mno Edson, hakuamini kama duniani kulikuwa na mtu aliyekuwa na roho mbaya kama alivyokuwa Edson, kila siku maisha yake yalikuwa ni kusali tu, yaani Edson apate matatizo, augue ugonjwa usiopona au kama itawezekana afe kabisa.
Hilo likawa kama dua la kuku, kamwe halikumpata mwewe, wakati akiomba Edson apate matatizo au afe ndiyo kwanza mwanaume huyo alizidi kufanikiwa na kuwa bilionea mkubwa.
Siku zikakatika, miezi ikaenda mbio na miaka nayo kusogea, muda haukumsubiri mtu. Baada ya miaka mitano, ndiyo kwanza mtoto wake, Cynthia alikuwa na miaka kumi.
Shule aliyokuwa akisoma ilikuwa ni shule za watu masikini ambazo zilijulikana kama Kayumba. Huko, alionekana kuwa na mawazo mno, ndiyo kwanza alikuwa darasa la tatu lakini kwa jinsi mama yake alivyokuwa na huzuni kila siku, kukamuathiri, akawa na mawazo lukuki kiasi ambacho kila siku alionekana kutokuwa na furaha kabisa.
“Cynthia, tatizo nini mwanangu?” aliuliza mwalimu Asha, aliamua kumuita Cynthia kwa lengo la kumuuliza kwani kila siku mtoto huyo hakuwa na furaha kabisa.
“Hakuna kitu mwalimu.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Hakuna kitu.”
Japokuwa alijitetea sana lakini bado walimu walijua kwamba kulikuwa na tatizo ambalo mtoto huyo hakutaka kuliweka wazi. Walitaka kujua kwani hali ile ilimfanya mpaka kufanya vibaya darasani.
Walichoamua kama walimu ni kumuagiza kumuita mama yake, kesho akafika naye shuleni hapo. Anita alikonda sana, alivyoonekana kwa walimu wale, walihisi kwamba mwanamke huyo alikuwa mgonjwa, tena wa wa kifua kikuu kilichokomaa ambao waliishi katika hatua za mwisho za kuvuta pumzi ya dunia hii.
Walimu walishtuka mno, hawakuamini kama kweli yule alikuwa mama yake Cynthia, mtoto mrembo aliyemvutia kila mtu aliyemwangalia. Alipofika mbele ya walimu hao, Anita akaanza kukohoa mfululizo, hiyo ilionyesha kwamba alikuwa akiumwa, hivyo wakamchukua na kumpeleka ofisini.
“Wewe ni nani?” aliuliza mwalimu Asha, ndiye alikuwa mwalimu wa darasa wa Cynthia.
“Mama yake Cynthia.”
“Unaitwa nani?”
“Anita.”
“Kuna kitu kinaendelea nyumbani kwako?”
“Kitu gani?”
Alichokifanya mwalimu ni kumwambia Cynthia aende nje ya ofisi ile kisha wao kama walimu kuanza kuzungumza na Anita. Mwanamke huyo hakutaka kuwaficha, alichokifanya ni kuwahadithia kila kitu kilichotokea maishani mwake tangu alipokuwa na mumewe, alipofariki katika ajali ya boti ya Royal Palm, alipokuja kuwa na Edson mpaka kumuacha na kumdhulumu mali zake.
“Huyuhuyu Edson Kambani au?”
“Ndiye huyohuyo! Alichukua kila kitu kutoka kwangu,” alijibu Anita.
“Hapana! Haiwezekani!”
“Kweli tena!”
“Labda useme kingine lakini si hicho,” alisema mwalimu mmoja.
Hakukuwa na aliyemwamini, walimfahamu Kambani, alikuwa mmoja wa watu waliosaidia sana jamii, alikuwa tayari hata yeye kulala njaa lakini mwisho wa siku watu waliokuwa na shida wapate chakula.
Kitendo cha Anita kusema kwamba mali alizokuwa nazo Kambani zilikuwa zake, hakukuwa na mtu aliyemwamini hata kidogo , tena ndiyo kwanza walimu haohao walimsuta.
Anita aliumia moyoni mwake, hakuamini kama hakuaminika hata kidogo, kilichobaki ni kuumia moyoni mwake, hakuamini kama watu hao walifikia hatua ya kumwamini sana Kambani kiasi kwamba hata aliposema kwamba mwanaume huyo alimdhulumu mali yake, hakukuwa na aliyemwamini hata kidogo.
Akaondoka shuleni hapo huku akilia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, walimu wale badala ya kumfariji kutokana na matatizo aliyokuwa akipitia ndiyo kwanza walimsabababishia maumivu makubwa moyoni mwake.
Wakati amefika barabarani, kituoni kwa ajili ya kuchukua daladala kurudi nyumbani, ghafla, gari moja lisilokuwa na namba likasimama mbele yake. Hata kabla hajajiuliza lilikuwa gari la nani, mara vijana wanne waliokuwa na bunduki mikononi wakateremka na kumfuata.
Watu waliokuwa karibu naye wakapigwa na taharuki, hawakujua watu wale walikuwa wakina nani. Wakati raia walipojaribu kutaka kumsaidia Anita, risasi kadhaa zikapigwa hewani, wote waliokuwa mahali hapo wakakimbia.
Anita akachukuliwa na kupakizwa ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea asipopafahamu. Mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda, hakujua watu hao walikuwa wakina nani na walihitaji nini. Alipojaribu kuuliza, akapigwa vibao viwili mfululizo kama ishara ya kuonyeshwa kwamba watu hao hawakuhitaji maswali yoyote yale. Akabaki kimya.
*****
Kilichokuwa kimepangwa ni kumuua Anita tu, Edson Kambani alijipanga, hakutaka kusikia kitu chochote kile, alichoambiwa kwamba mwanamke huyo alikuwa hatari na hivyo alitakiwa kumuua haraka iwezekanavyo.
Akawatuma vijana wake kwa ajili ya kukamilisha kazi ambayo kwake ilionekana kuwa kubwa, alitulia nyumbani huku mara kwa mara macho yake yakiwa kwenye simu yake kwani alitegemea muda wowote ule angepokea simu kutoka kwa vijana wake wakimpata taarifa ya ushindi mkubwa.
Aliisikilizia simu ile mpaka pale aliposikia ikiita, kwa harakaharaka akaichukua na kuipeleka sikioni ambapo sauti ya mwanaume kutoka upande wa pili ikaanza kusikika.
“Tumekamilisha mkuu! Nini kinafuata?” aliuliza mwanaume huyo.
“Mpo naye?”
“Ndiyo mkuu! Tunasikia neno lako tu, kama kumuua au la.”
“Nyie muueni tu, hakuna zaidi ya hilo,” alisema Kambani huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
Vijana wale waliokuwa na Anita waliendelea na safari yao, mwenzao alipokuwa akizungumza kwa simu na kupewa maagizo kwamba Anita alitakiwa kuuawa, nao walisikia ila wakawa wanahitaji kusikia zaidi kama kweli kile walichokisikia ndicho walichoagizwa au la.
Anita alibaki akitetemeka, kila alipowaangalia vijana wale, walionekana kama walikuwa maadui zake ila hakujua ni nani aliwatuma kwa ajili ya kummaliza. Kichwa chake kilikuwa na maswali mengi, hata simu ilipopigwa na mwanaume mmoja kuzungumza na huyo mtu aliyejifanya kuwa bosi, alijitahidi kuisikiliza sauti hiyo ili kuona kama aliitambua lakini aliambulia patupu.
“Bosi kasemaje?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Tumuue tu.”
“Hakuna noma.”
Anita alivyosikia hivyo, akachanganyikiwa, akaanza kulia kwa uchungu mkubwa. Aliogopa kuzungumza lolote lile kwani bado alikumbuka vema lile kofi alilopigwa dakika chache zilizopita.
Vijana wale hawakuzungumza kitu chochote kile zaidi ya kuanza kuzikoki bastola zao tayari kwa kufanya mauaji mbele ya safari kwani piga ua ilikuwa ni lazima Anita auawe kikatili.
Wakati huo gari lilikuwa likielekea katika Msitu wa Pande. Njiani, walikuwa wakizungumza tena kwa kupongezana kwa kazi kubwa waliyoifanya na baada ya muda wangeikamilisha na hivyo kugaiwa kiasi cha fedha kilichobaki.
“Jamani nimewafanya nini?” aliuliza Anita, aliona kama kupigwa, acha apigwe lakini ilikuwa ni lazima ajue alichokifanya mpaka kutekwa.
“Nilikwambiaje?” aliuliza mwanaume yule aliyempiga mara ya kwanza.
“Jamani! Mnanionea, sijamfanya mtu kitu chochote, nimetoka kumpeleka binti yangu shule, jamani, nimef…” alisema Anita lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake akakatishwa na sauti nzito ya kiume.
“Nyamazaaa…hayo maswali utamuuliza Kambani mkikutana ahera, sisi tunakamilisha kile alichotuagiza,” alisema mwanaume huyo.
Hapo ndipo Anita alipopata jibu ya kile kilichokuwa kikiendelea, moyo wake uliumia mno kwani kitendo cha kuambiwa kwamba mtu aliyekuwa nyuma ya tukio hilo alikuwa Kambani kilimshtua sana.
Alijua kwamba mwanaume huyo ndiye aliyemdhulumu mali zote na kisha kumfukuza, sasa ilikuwaje mpaka leo hii bado alikuwa akimtafuta na kutaka kumuua? Miaka saba ilipita, leo hii aliwatuma watu ili wakamuue, akajikuta akimchukia zaidi.
“Jamani! Hivi nimemfanya nini Edson…jamani, nimemfanya nini mimi? Kanidhulumu mali zangu, bado hajaridhika mpaka kutaka kuniua?” aliuliza Anita huku akilia kama mtoto.
Hakukuwa na mtu aliyeongea kitu chochote kile, walichokifanya ni kuendelea na safari yao. Mara baada ya kupita Mbezi Mwisho, wakaendelea mbele zaidi kuufuata msitu wa Pande, walipokwenda kwa umbali fulani, wakawa wamekwishakaribia.
“Simamisha gari kwanza,” alisema mwanaume mmoja mwenye sauti ya uongozi. Gari likasimamishwa.
“Tumuueni hapahapa au tuingia ndani ya msitu?” aliuliza mwanaume huyo.
“Tungeingia ndani ya msitu, hapa noma,” alisema mwanaume mmoja.
“Basi poa, liingize gari ndani.”
Wakati dereva akiwa amekwishapiga gia tayari kwa kuingia msituni, ghafla mlio mkubwa ukasikika nyuma, gari lile walilokuwemo likagongwa kwa nyuma na gari lililoonekana kuwa kwenye mwendo wa kasi.
“Puuuuuu…” mlio huo wa kugongwa ulisikika.

Kwa kuwa dereva hakuwa amefunga mkanda, akajikuta akikigonga kichwa chake katika kioo cha mbele, wale wanaume wengine nao wakarushwa mpaka mbele ya gari lile na kujibamiza kwenye kioo kile ila kwa kuwa Anita aliwekwa chini, hata lile gari lilipogongwa, hakwenda mbele, alijigonga kwenye kiti cha mbele tu kitu ambacho hakikumletea hata maumivu yoyote yale.

Huku kila mmoja akiwa anaugulia maumivu, mara wanaume watatu waliokuwa na bunduki mikononi mwao wakatokea mahali hapo, wakaufungua mlango mkubwa wa gari lile na kisha kuanza kuwamiminia risasi wanaume waliokuwa ndani ya gari lile.

Anita ambaye alikuwa amechanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, alijikuta akiikutanisha mikono yake na kuanza kumuomba Mungu ili amuokoe na kile kilichokuwa kikiendelea garini mule.

Alitetemeka mpaka kujisaidia haja ndogo pale alipokuwa. Wanaume wale wakaanza kuangalia huku na kule ndani ya gari lile, walikuwa wakimtafuta Anita aliyekuwa humo, walipomuona, wakamshika mkono na kuanza kumtoa kinguvu.

“Let’s get out of here,” (Tuondoke hapa) alisema mwanaume mmoja kwa Kiingereza.

“Who are you? What have I done to you?” (Nyie ni wakina nani? Nimewafanya nini?) aliuliza Anita.

“Don’t ask any question, you have to do what we want you to, otherwise, we’ll kill you,” (Usiulize swali lolote, unatakiwa kufanya tunachotaka ukifanye, vinginevyo tutakuua) alisema mwanaume huyo. Anita akabaki kimya.

Walichokifanya ni kumchukua na kisha kuondoka naye mahali hapo. Ndani ya gari, bado Anita alikuwa akitetemeka, watu wale waliokuwa ndani ya gari lile walionekana kama si Watanzania kwani muda mwingi wa mazungumzo yao walikuwa wakizungumza Kiingereza tu.

Mbali na hilo, hata ngozi zao hazikuonyesha kama walikuwa Watanzania, walionekana kama watu kutoka katika nchi za Uarabuni waliokuwa na wazazi wenye mchanganyiko wa rangi.

Anita hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, alijiuliza maswali mengi kuhusu watu hao lakini hakupata jibu lolote lile. Aliokolewa kwenye hatari ya kuuawa na watu hao lakini bado hakuwa na uhakika kama watu hao walikuwa watu wema kwake au watu wabaya.

“Who are you?” (Nyie ni wakika nani?)

“Calm down, we are good people to you,” (Tulia, sisi ni watu wema kwako) alisema mwanaume mmoja.

Anita hakuweza kunyamaza, muda wote alikuwa na hofu moyoni mwake, japokuwa aliambiwa na watu hao kwamba asiwe na wasiwasi wowote lakini hilo halikutosha kumfanya kujiachia ndani ya gari hilo.

Gari lilikwenda mpaka lilipofika Magomeni Mapipa alipokuwa akiishi na wazazi wake, gari likasimama nje ya nyumba hiyo na kumtaka kuteremka. Kwa kuwa gari lilikuwa na vioo vyeusi, hakugundua hapo kulikuwa wapi ila aliposhuka na kugundua kwamba palikuwa nyumbani kwao, akashtuka.

“Imeakuwaje tena? Nyie ni wakina nani?” aliuliza Anita huku akionekana dhahiri kuchanganyikiwa.

“Usijali! Nenda nyumbani! Kuwa makini, watu wabaya bado wanakutafuta. Tutakufuata wiki ijayo, tunakutafutia nyumba na utakwenda kuishi huko,” alisema mwanaume mmoja.

“Nyie ni wakina nani lakini?” aliuliza Anita kwa mshangao.

“Tulikwambia sisi ni raia wema. Anita! Roho yako inahitajika sana, ila usijali, tutakulinda wewe na mtoto wako,” alisema mwanaume yule.

“Sawa! Nani anataka kutuua?”

“Edson Kambani.”
Watu wale hawakutaka kuzungumza zaidi, walichokifanya ni kuondoka mahali hapo huku wakisisitiza kwamba ilikuwa ni lazima wamlinde mwanamke huyo na mtoto wake.

Bado Anita alibaki kuwa na maswali mengi, watu wale walimshangaza sana, hakuwafahamu, hakujua ni wakina nani na walihitaji nini na kwa sababu gani waliamua kumlinda.

Hakutaka kulipuuzia suala hilo, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake ambao hata nao pia wakaonekana kushtuka sana.

“Haiwezekani! Ni wakina nani hao?” aliuliza baba yake.

“Hata mimi siwajui, ila ni watu wazuri nahisi.”
“Mhh! Nina wasiwasi! Isije ikawa wanakutengenezea mazingira mazuri ya kukuua!” alisema mama yake.

“Sidhani mama! Ngoja niendelee kupeleleza nijue ni wakina nani,” alisema Anita huku akiingia chumbani mwake, kichwa chake kilichanganyikiwa mno.

*****

Kambani alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokuwa akikiangalia kwenye televisheni kwamba watu aliokuwa amewatuma, walikutwa wameuawa Mbezi ya Kimara huku miili yao ikiwa imepigwa risasi.

Aliiangalia televisheni ile na kuwasikiliza mashuhuda wa tukio hilo ambalo walilieleza tukio kwa ujumla kwamba gari hilo lilisimamishwa pembeni mwa msitu na baada ya muda kulikuwa na gari jingine ambalo liliigonga gari hilo kwa nyuma.

Baada ya tukio hilo, wanaume watatu wakateremka na kulifuata lile gari kisha kuwapiga risasi watu hao na kuondoka na mwanamke ambaye hakuweza kujulikana.

Kambani hakujua hao watu walikuwa wakina nani, alijua dhahiri kwamba mwanamke huyo alikuwa Anita, kitu kilichomsumbua kichwani mwake ni juu ya watu hao, kwa nini waliamua kuwaua vijana wake? Kila alichojiuliza, alikosa jibu kabisa.

Alichokifanya ni kuwapigia simu mabilionea wenzake kwa ajili ya kuzungumza nao, alitaka kuwaambia kila kitu kilichotokea ili kujua kama alitaka kuchukua hatua ya pili kumuua Anita, alitakiwa kufanya nini.

Baada ya dakika ishirini, mabilionea wenzake wawili wakafika nyumbani hapo, wakaweka kikao kidogo kwa ajili ya kushauriwa ni kitu gani kilitakiwa kufanyika mahali hapo kwani kwa jinsi ilivyoonekana, watu waliowaua vijana wake walikuwa hatari sana.

“Ila wao ni wakina nani na kwa nini waliamua kuondoka na Anita?” aliuliza Marimba huku akimwangalia Kambani usoni.

“Hilo ni swali linaloniumiza sana kichwa changu,” alijibu Kambani.

“Au naye alikuwa na mtandao mkubwa wa vijana wa kazi?” aliuliza Nkone.

“Sidhani! Hilo sijui kama lilikuwepo. Ninachojua ni kwamba alikuwa akiishi na mumewe, alifariki katika ile ajali ya boti iliyotokea miaka ileeee…” alisema Kambani.

“Sasa hao watu walitoka wapi?”

“Hapo ndipo kunaponichanganya.”

Kama yeye alivyochanganyikiwa ndivyo ambavyo hata wenzake walivyochanganyikiwa. Kichwa chake hakikutulia, kila wakati alijaribu kufikiria tukio hilo lakini hakupata jibu kabisa.

Alichotaka ni kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba Anita anauawa kwa gharama zozote zile. Akawatafuta vijana wengine kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo ambayo kwa kipindi cha nyuma ilishindikana kufanyika.

Akawapa maelekezo juu ya mahali alipokuwa akiishi Anita na kwa namna gani wangeweza kumpata. Vijana hao walikuwa wanne, walioonekana kuwa na ubavu wa kumpata mwanamke huyo.

Kabla ya kufanya kazi akawalipa kabisa nusu ya malipo waliyokuwa wakiyahitaji kisha kazi kubaki kwao tu. Waliambiwa tu kwamba walitakiwa kuwa makini kwani kwa namna moja au nyingine, mwanamke huyo alionekana kuwa na ulinzi wa kutosha.

“Hilo si tatizo mkuu!” alisema mwanaume mmoja.

“Basi sawa! Nendani.”

ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA

Facebook Comments

Tags
Show More

Related Articles

Close