Simulizi

Niliua Kumlinda Mama Yangu – 07

Kabla ya kufanya kazi akawalipa kabisa nusu ya malipo waliyokuwa wakiyahitaji kisha kazi kubaki kwao tu. Waliambiwa tu kwamba walitakiwa kuwa makini kwani kwa namna moja au nyingine, mwanamke huyo alionekana kuwa na ulinzi wa kutosha.
“Hilo si tatizo mkuu!” alisema mwanaume mmoja.
“Basi sawa! Nendani.”
Kambani alitulia nyumbani na mabilionea wenzake. Wote walionekana kuwa na wasiwasi, hawakujua hao watu waliokuwa wakimsaidia Anita walikuwa ni wakina nani na kwa nini walifanya hivyo.
Ndani ya nyumba hiyo, muda mwingi waliutumia kuwa kimya na si kuzungumza, kama walihitaji kujadili kitu fulani, walifanya hivyo lakini kwa dakika chache mno.
Ilipofika jioni, kazi ya Kambani ilikuwa ni kusikilizia simu, alitaka kuona kama vijana wale wangempigia simu na kumpa taarifa nzuri au ndiyo ingekuwa kama ilivyokuwa kwa wale vijana wengine.
Alisubiri simu, dakika zilikwenda mbele, saa zikasogea lakini hakukuwa na simu yoyote ile iliyopigwa ambayo ilitoka kwa vijana wale. Ilipofika saa tatu usiku, simu yake ikaanza kuita, kwa haraka sana akaichukua na kuangalia kioo, namba ya mmoja wa watu wale aliokuwa akiwasikilizia ndiyo ambayo ilikuwa ikiingia muda huo. Kwa harakaharaka akapokea.
“Vipi huko?” aliuliza hata kabla ya salamu.
“Mkuu! Wenzangu wote wameuawa kwa kupigwa risasi,” alisema kijana huyo kwenye simu.
“Wameuawa! Na nani?”
“Na hawa jamaa walioniteka,” alijibu kijana huyo.
“Wakina nani? Ni Watanzania?”
“Sidhani! Waongea sana Kiingereza. Wameniambia nikupigie simu, nipo nao hapa wameniweka chini ya ulinzi,” alisikika kijana huyo.
“Hebu wape simu nizungumze nao,” alisema Kambani. Baada ya sekunde tatu, akarudi hewani.
“Wamekataa mkuu! Ila wanachokisema ni kwamba uache kumfuatilia Anita la sivyo watakuua wewe pia, Marimba na Nkone,” alisema kijana huyo maneno yaliyowafanya mabilionea wote kushtuka.
“Unasemaje?” aliuliza Kambani huku akiwa amechanganyikiwa.
“Paaaa….paaaa….” milio ya risasi ikasikika upande wa pili iliyoonyesha kwamba kijana huyo alipigwa risasi.
“Haloo…halooo….” aliita Kambani lakini hakukuwa na majibu yoyote yale kutoka upande wa pili. Mbaya zaidi, simu ikakatwa.
Mabilionea hao walichanganyikiwa, hawakuamini kilichotokea, vijana waliowatuma ambao waliwaahidi kwamba wangeifanya kazi, ripoti iliwafikia na kusema kwamba watu hao wote waliuawa na tena huyo mmoja wa mwisho aliuliwa huku wakisikia.
Kitendo cha kuambiwa kwamba endapo wangeendelea kumfuatilia Anita wote watatu wangeuawa kiliwaogopesha, wakajaribu kujiuliza watu hao walikuwa wakina nani lakini hawakupata jibu.
Katika maisha yao hawakuwahi kuwa na uhasama na mtu yeyote yule, tena kitu kilichowashangaza sana ni pale mtu huyo aliposema kwamba watu hao walionekana kama siyo Watanzania, sasa kama si Watanzania, walikuwa wakina nani, walipataje taarifa za wao kutaka kumuua Anita na kwa nini walimsaidia mwanamke huyo? Kila walichojiuliza, walikosa jibu.
“Siwezi kukata tamaa ndugu zangu,” alisema Kambani huku akionekana kumaanisha alichokisema.
“Kuhusu kumuua Anita?”
“Ndiyo! Ni lazima nimuue kwani anaweza kuwa tatizo huko mbele.”
“Ila umesikia mkwara?”
“Nimesikia, unafikiri kama sitomuua Anita, nini kitatokea? Ni lazima nitapata usumbufu huko mbele,” alisema Kambani.
“Kwa hiyo?
“Nimepata wazo.”
“Lipi?”
“Tumteke mtoto wake, tukifanikiwa katika hilo, tutakuwa tumefanikiwa kumpata hata yeye mwenyewe na kisha kumuua, ni rahisi sana,” alisema Kambani wazo lililokubaliwa na kila mtu. Harakati za kumteka mtoto zikaanza.
*****
“Mtoto mzuri unaitwa nani?” aliuliza mwanaume mmoja, alikuwa amemsimamisha Cynthia mbele yake.
“Naitwa Cynthia.”
“Unasoma wapi?”
“Shule hiyo hapo.”
“Darasa la ngapi?”
“La tatu.”
“Hongera sana.”
Binti mdogo Cynthia alikuwa akizungumza na mwanaume aliyesimama mbele yake ambaye kwa kumwangalia ungeweza kusema kwamba alikuwa mtu mwema.
Hatua kumi kutoka pale walipokuwa lilisimamishwa gari moja lililokuwa na vioo vyeusi. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi na mwanaume huyo kutokana na muonekano mzuri aliokuwa nao.
Kijana yule aliendelea kuzungumza na binti huyo kwa dakika kadhaa huku akiuliza maswali mfululizo. Cynthia hakufahamu kitu chochote kile, kila alichoulizwa, alikijibu tena ka ufasaha kabisa.
Baada ya dakika kadhaa, wanaume wengine wawili wakateremka kutoka ndani ya gari lile na kuanza kupiga hatua kule mwenzao aliposimama na Cynthia, walipofika, hawakutaka kuongea kitu chochote zaidi ya kumchukua msichana huyo, wakambeba na kuanza kuondoka naye.
Kila mtu aliyekuwa mahali pale alishtuka, hawakuelewa kilichokuwa kikiendelea, walijaribu kuwaangalia watu wale vizuri, wote walikuwa wameshika bastola, hawakutaka kupiga risasi hewani, walichokifanya ni kuelekea katika gari lile, wakaingia na kuondoka zao.
“Mwalimu….” alisema mwanafunzi mmoja, alikuwa ametoka mbiombio mpaka shuleni, akaingia katika ofisi ya walimu.
“Unasema Halima.”
“Cynthia amechukuliwa na wanaume nje,” alisema Halima.
“Cynthia?”
“Ndiyo! Amechukuliwa na wanaume hapo nje, twendeni mkaone,” alisema Halima.
Walimu wote waliokuwa ndani ya ofisi ile wakatoka nje na kuondoka na mwanafunzi huyo mpaka nje ambapo wakakutana na kundi kubwa la watu waliokuwa wakizungumzia kuhusu tukio lile lilivyokuwa.
Wakauliza kilichokuwa kimetokea na mwanaume mmoja kuelezea mchezo mzima ulivyokuwa, yaani pale Cynthia alipofuatwa na mwanaume mmoja, alipozungumza naye mpaka pale wanaume wengine wawili walipokuja na kumchukua kisha kuondoka naye.
“Mnasema walikuwa na bastola?”
“Ndiyo! Walionekana kuwa na roho ya kikatili sana, tuliogopa hata kuwafuata,” alisema mwanaume huyo.
“Wamekwenda wapi?”
“Upande huu, ila hatujui sehemu gani.”
Walimu wakaanza kwenda kule lilipokwenda gari lile kwa kuamini kwamba wangeweza hata kuliona, njia nzima ilikuwa nyeupe. Walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, walichokifanya ni kumpigia simu Anita na kumwelezea kile kilichokuwa kimetokea.
“Unasemaje?” ilisikika sauti ya Anita huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Kuna taarifa mbaya juu ya mwanao.”
“Taarifa gani mwalimu.”
“Njoo shule.”
Anita alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokisikia kwamba kulikuwa na taarifa mbaya juu ya mwanaye, kitu kilichokuja kwa haraka sana kichwani mwake ni kwamba mtoto wake alikuwa akiumwa au hata kufariki dunia.
Joto la mwili wake likaongezeka, mapigo ya moyo yakaanza kumdunda kwa nguvu, alihisi miguu ikikosa nguvu na hata wakati mwingine kujiona kama angefariki dunia kutokana na presha kubwa aliyokuwa nayo.
Akatoka mpaka kituoni ambapo akachukua daladala na kuelekea mpaka shuleni kwa mtoto wake, huko, alielekea mpaka ofisini, hata kuvaa kitambaa kichwani alisahau, nywele zilikuwa timtim.
“Mwanangu yupo wapi?” aliuliza Anita mara baada ya kuingia ofisini, hata salamu hakutoa.
“Subiri kwanza.”
“Ninataka kumuona mwanangu, niambieni yupo wapi,” alisema Anita huku akilia kama mtoto.
Ilikuwa ni vigumu kumwambia kile kilichotokea kwani kila walipotaka kufanya hivyo, mwanamke huyo alikuwa akilia tu. Wakaanza kumbeleza, walimtaka anyamaze kwanza na ndipo wamwambie kile kilichokuwa kimetokea.
Haikuwa kazi rahisi kunyamaza, baada ya dakika kadhaa ndipo akanyamaza na hivyo walimu kuanza kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Hawakuacha kitu, hakukuwa na haja ya kuficha, walisimulia kila kitu.
“Jamani…Kambani nimemfanya nini huyu…mbona ananitafuta hivi…” alisema Anita huku akilia kama mtoto.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kusema kuhusu Kambani, zilikuwa tuhuma nzito zilizowafanya walimu kutokuelekea kile kilichokuwa kikiendelea. Walimfahamu Kambani, alikuwa mwanaume tajiri aliyekuwa radhi kuwasaidia watu wengi kwa kutumia utajiri mkubwa aliokuwa nao.
Kitendo cha Anita kusema mara ya pili kwamba Kambani ndiye alikuwa nyuma ya kila kitu kiliwachanganya walimu wote, ilibidi wamuulize ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea kwani kwa kile walichokijua ni kwamba mwanaume huyo alikuwa mtu mwema ambaye alikuwa tayari hata kutumia senti yake ya mwisho kwa ajili ya watu wengine.
“Ila kuna nini kati yako na Kambani?” aliuliza mwalimu mmoja.
“Hakuna kitu.”
“Sasa kwa nini kila wakati unamtajataja tu, sijui kakutapeli, mara kakuibia mtoto wako, hivi kuna nini kinaendelea?” aliuliza tena mwalimu huyo.
“Hakuna kitu mwalimu. Nataka niende polisi,” alisema Anita.
Hakuwa na jinsi, alichokifikiria ni kwenda polisi kutoa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea. Hata polisi wenyewe walichanganyikiwa, hakukuwa na taarifa za utekaji nyara kwa watoto tena kutoka katika familia masikini kama alivyokuwa Anita, walishangaa, hawakujua hayo watekaji walihitaji nini.
Walichokifanya polisi hao ni kuandika maelezo ya Anita katika faili lao kisha polisi wengine kwenda kwenye eneo la tukio na kuanza kufanya upelelezi wao, walitaka kufahamu ni kitu gani kilitokea, gari lilielekea upande gani, walichokiamini ni kwamba wangefanikiwa kumpata Cynthia.
*****
“Bosi! Tumekwishampata huyu mtoto! Kwa hiyo?” aliuliza kijana mmoja.
“Mpelekeni sehemu salama mmuhifadhi!”
“Sawa. Tunampeleka kambini kwetu, ukimhitaji utampata hukohuko.”
“Sawa. Nipeni dakika arobaini na tano nitakuwa huko.”
“Sawa.”
Wakati huo gari lilikuwa likiendeshwa kwa kasi kuelekea Tandale. Mara baada ya kumteka Cynthia, watekaji hao walimchukua, wakampakiza garini na kisha kuanza safari ya kuelekea Tandale kwa Mtogole ambapo ndipo kulipokuwa na kambi yao.
Muda wote Cynthia alikuwa akilia, alimlilia mama yake, alitaka kuachwa ili arudi nyumbani kuungana na mama yake. Kila alipowaangalia wanaume hao, hakukuwa hata na mtu mmoja aliyekuwa akimfahamu, wote hao walikuwa wageni kwake.
Moyoni mwake alijua kwamba watu hao walikuwa watu wabaya hivyo kulia kwake kuliendana na uoga aliokuwa nao moyoni mwake kwa kuogopa kuuawa na watu hao ambao walionekana kuwa katili.
Gari lilipofika kwa Mtogole, likakata kushoto na kuchukua barabara iliyokuwa ikienda Tandale Sokoni, walipandisha nayo mpaka kulipokuwa na makaburi ya Bi Mtumwa, wakaenda mbele, wakakutana na msikiti ambapo hapo wakakata kushoto.
Kuanzia hapo, gari halikwenda umbali mkubwa, likasimama na kisha kumteresha Cynthia na kuanza kuondoka naye kuelekea uchochoroni.
“Pudi! Baki na gari, tunakuja,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa akimwambia mwenzao.
“Poa, fanyeni shuta basi,” alisema Pudi.
“Poa.”
Pudi akabaki garini, alijifungua ndani huku ni kiyoyozi tu ndicho kilichokuwa kikipuliza. Huku akiwa kwenye utulivu mkubwa ndani ya gari, akasikia kioo cha mlango wa mbele kikigongwa, akachungulia nje, macho yake yakatua kwa msichana mrembo aliyekibusti kifua chake na kumtamanisha mwanaume yeyote ambaye angemuona, Pudiakafungua kioo kile kwa lengo la kumsikiliza.
Hapohapo akiwa amejisahau huku amechanganyikiwa na uzuri wa msichana huyo, wanaume wawili waliokuwa na mchanganyikio wa rangi wakatokea ghafla, wakampiga kitako cha bunduki usoni, Pudi akaangukia kitini ndani ya gari, wanaume hao wakaingia ndani na kutulia .
Wale watekaji wawili waliokuwa wameondoka na Cynthia waliporudi, moja kwa moja wakafungua milango na kuingia ndani pasipo kugundua kwamba humo ndani kulikuwa na wanaume wengine waliokuwa wameingia.
Walipokaa vitini tu, wakashtukia wakiwekwa chini ya ulinzi na kuamriwa kutulia vinginevyo wangepigwa risasi wote.
“Put your hands where we can see them,” (Wekeni mikono yenu tuione) alisema mwanaume mmoja na watekaji hao kufanya hivyo huku wakitetemeka.
Kilichotokea ni kufungwa kamba humo garini kisha kumchukua mwanaume mmoja na kumtaka awaongoze mpaka kule walipomuweka Cynthia. Kwa kuwa aliwahiwa kuonyeshewa bunduki tena na watu ambao wala hakuwafahamu, akafuata masharti hivyo kuteremka na kuanza kuwaongoza kule walipomuweka Cynthia.
Walipofika kwenye nyumba moja, wakaingia ndani, mule, wakamkuta Cynthia akiwa analia tu, muda wote aliwaambia watu hao kwamba alitaka kumuona mama yake.
“Who sent you?” (Nani aliwatuma) aliuliza mwanaume mmoja.
“Edson Kambani.”
“Where is he?” (Yupo wapi?)
“He is on the way,” (Yupo njiani anakuja)
Walichokifanya ni kumsubiria vitini kwa kuamini kwamba ilikuwa ni lazima kuja mahali hapo. Hawakutaka kuzungumza kitu chochote kile, walikaa huku bastola zikiwa mikononi mwao, walionekana kuwa na hamu ya kukutana na mwanaume huyo ambaye walikwishawahi kuzungumza naye waachane na Anita lakini hakuonekana kuelewa kitu chochote kile.
Baada ya nusu saa, Kambani akafika mahali hapo, alipofungua mlango na kuingia ndani, akamkuta kijana wake akiwa amewekwa chini ya ulinzi na watu asiowafahamu lakini aliwahi kuwasikia kutoka kwa kijana wake aliyepigwa risasi wakati akizungumza naye kwenye simu.
“Please dont kill me…” (Tafadhalini, msiniue…) alisema Kambani mara baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo.
“We can’t kill you, this is the one who will kill you,” (Hatuwezi kukua, huyu ndiye atakayekuua) alisema mwanaume mmoja huku akimnyooshea kidole Cynthia kwamba ndiye atakayemuua Kambani.
“Please…” (Tafadhalini)
“She won’t kill you today,” (Hatoweza kukuua leo) alisema kijana mmoja.
Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka na Cynthia kurudi garini tayari kwa kuanza safari yao ya kuelekea kule walipotoka.
Ndani ya nyumba ile, Kambani alichanganyikiwa, hakuamini kama kweli alinusurika kuuawa na watu hao walioonekana kuwa si Watanzania, walikuwa kama Wapemba kutokana na mchanganyikio wa ngozi waliokuwa nao.
Akawaangalia vijana wake, hakuamini kama kweli walishindwa kukamilisha kile alichowaagiza, kitendo cha Anita na Cynthia kuwa hai bado kilimuumiza moyo wake kwani alijua fika kwamba hapo baadaye angeweza kupata matatizo au hata kupokonywa utajiri mkubwa aliokuwa nao.
“Mlishindwaje?” aliuliza Kambani huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Tulivamiwa, ila wanaonekana si watu wabaya sana, ila kwa kuwatazama, wanaonekana kuwa na mafunzo makubwa sana ya kikomandoo,” alisema kijana mmoja.
Ndani ya gari, vijana wale wa Kipemba wakaondoka zao kuelekea nyumbani kwa Anita alipokuwa akiishi. Kwa sababu walikuwa na namba ya mwanamke huyo, wakampigia na kutaka kuonana naye kwani walikuwa na mtoto wake ambaye alitekwa na Kambani.
“Mpo wapi nije?” aliuliza Anita.
“Subiri, tutakushtua, ila ukija usije na polisi, kama tulivyokwambia kwamba tuna kazi ya kukulinda wewe na mtoto wako, hivyo usiwe na hofu yoyote ile” alisema jamaa mmoja.
Walipokwenda ilikuwa ni ndani ya gesti moja iliyokuwa Kinondoni, hapo, wakaingia na kupumzika na ndipo walipompigia simu Anita kwa lengo la kukutana naye.
Ndani ya dakika ishirini, mwanamke huyo alikuwa ndani ya gesti hiyo. Kitu cha kwanza akamkumbatia binti yake, hakuamini kama alikuwa hai, kila alipomwangalia, akajikuta akilia kwa furaha, swali lililomsumbua lilikuwa moja tu, watu hao walitumwa na nani na kwa nini walimlinda.
“Nyie ni wakina nani?”
“Hauwezi ukatufahamu, ila tulitumwa tukulinde,” alisema kijana mmoja.
“Mmetumwa mnilinde, na nani?”
“Unamfahamu Phillip Mnyome?” aliuliza kijana mmoja.
Anita alipolisikia jina hilo, akashtuka, machozi yakaanza kumtoka kwani moyo wake ulikumbushwa mbali kabisa. Huyo alikuwa mume wake, aliyempenda mno, alikufa baharini walipokuwa wakielekea Unguja.
Kitendo cha kuambiwa jina hilo tu, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa filamu, siku ambayo boti ya Royal Palm ilipozama na watu wengi kufa akiwemo mume wake. Moyo wake ulijaa maumivu makali kwani na ndiyo siku hiyohiyo alipokutana na Edson na kusababisha yote yaliyotokea.
“Ni mume wangu….” alijibu Anita.
“Huyo ndiye aliyetutuma…” alisema kijana mmoja.
“Mume wangu ndiye aliyewatuma?”
“Ndiyo! Anakupenda sana, amekuwa akikuzungumzia kila siku, amekuwa akikufuatilia kwa kipindi kirefu, anajua kila kitu kilichotokea, mpaka ulipodhulumiwa mali zako,” alisema kijana huyo.
“Mume wangu alikufa baharini, mwili wake hatukuuona hivyo tukazika nguo zake,”alisema Anita.
“Mumeo hakufa, yupo hai, anaishi. Alituagiza tuje tukulinde na Cynthia. Kwa sasa hivi, hataki mtoto wake aishi nchini Tanzania, anataka aende kule alipo yeye, kama kusoma, atasoma huko, na kila kitu, atafanyia huko,” alisema kijana huyo.
“Hapana! Siwezi kumuacha Cynthia aondoke mikononi mwangu, siwezi kuamini kama mume wangu yupo hai mpaka nizungumze naye,” alisema Anita.
“Hilo tu?”
“Ndiyo!”
Alichokifanya kijana huyo ni kuchukua simu yake na kisha kumpigia simu Phillip. Simu ikaanza kuita na kumpa Anita. Simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya mume wake kusikika.
Bado aliikumbuka sauti hiyo, alipoisikia, aligundua kwamba alikuwa mume wake, akajikuta machozi yakianza kumtoka, hakuamini kama mume wake ambaye kila siku alijua kwamba alikufa kumbe alikuwa hai.
“Halloo…” aliita Anita.
“Nakusikia mke wangu! Sauti yako haijabadilika. Bila shaka vijana wangu wameifanya kazi vizuri,” alisikika Phillip kwenye simu.
“Ndiyo! Nimekukumbuka mume wangu,” alisema Anita.
“Nimekukumbuka pia, pole kwa matatizo yote yaliyotokea, nilikuwa nyuma yako, nilihitaji kuilinda familia yangu, kweli nikafanya hivyo. Nilifanya hivyo kwa kuwa ninaipenda,” alisema Phillip.
“Ninahitaji kukuona, nataka nikuonea mpenzi.”
“Usijali, utaniona hivi karibuni. Ninataka Cynthia aje kuungana nami. Aje nilipo, nitamsomesha na kumfanyia kila kitu,” alisema Phllip.
“Ilikuwaje mpaka ukanusurika?”
“Ni stori ndefu. Ila sikutaka kujitokeza mapema kwa kuwa nilitaka ujifunze kwamba hautakiwi kumwamini kila mtu. Niliacha makusudi kwa kuwa nilijua kwamba yote yaliyotokea yangetokea,” alisema Phillip.
“Naomba unisamehe mume wangu.”
“Usijali. Mruhusu Cynthia aje huku. Atakuwa salama zaidi.”
“Hakuna tatizo. Ila upo wapi?”
“Kisiwani Madagaska.”
“Ninahitaji nikuone.”

Facebook Comments

Show More

Related Articles

Close