Simulizi

Niliua Kumlinda Mama Yangu – 08

“Ilikuwaje mpaka ukanusurika?”
“Ni stori ndefu. Ila sikutaka kujitokeza mapema kwa kuwa nilitaka ujifunze kwamba hautakiwi kumwamini kila mtu. Niliacha makusudi kwa kuwa nilijua kwamba yote yaliyotokea yangetokea,” alisema Phillip.
“Naomba unisamehe mume wangu.”
“Usijali. Mruhusu Cynthia aje huku. Atakuwa salama zaidi.”
“Hakuna tatizo. Ila upo wapi?”
“Kisiwani Madagaska.”
“Ninahitaji nikuone.”
“Usijali! Utaniona tu, utaniona hivi karibuni,” alisema Phillip na kisha kukata simu.
Walichokifanya vijana wale ni kumpa mfuko fulani mkubwa uliokuwa na fedha nyingi kama kianzio cha maisha yake mapya katika nyumba ambayo wao wenyewe waliamua kumtafutia huku ikiwa na kodi ya zaidi ya shilingi laki tano kwa mwezi.
Walipomaliza makabidhiano hayo wakaenda katika nyumba hiyo iliyokuwa Bunju, walimtaka kujificha yeye na wazazi wake kwani kwa jinsi walivyojua ilikuwa ni lazima siku moja Kambani amtafute mwanamke huyo na kumuua, na kama si hivyo basi ilikuwa ni lazima awaue hata wazazi wake, hivyo walimtaka kujificha.
*****
Boti ilikuwa ikizama, kila mtu alihangaika kuyaokoa maisha yake. Wengine walikuwa wakipiga kelele wakiomba msaada, kila walipoangalia pande zote, hakukuwa na dalili ya nchi kavu wala hakukuwa na dalili ya boti au meli yoyote ile.
Phillip hakutulia, alikuwa akihangaika huku na kule kuitafuta familia yake, hakutaka kuipoteza, kwa kipindi hiki, familia hiyo ilikuwa kitu muhimu kuliko chochote kile.
Hakujua sababu iliyomfanya mke wake kuondoka pale walipokuwa wamekaa, mawazo yake yalimwambia kwamba mwanamke huyo atakuwa na Edson tu kwani ndiye ambaye alikutana naye kwenye boti, aliifahamu historia nzima kwamba kipindi cha nyuma watu hao walikuwa wapenzi.
Hakufanikiwa kuiona familia yake, mawimbi yalipiga na boti ile kuanza kuzama. Moyo wake ukakata tamaa kwa kuona kwamba asingeweza kuiona familia yake tena.
Wakati boti ikiwa imezama, abiria wakiendelea kujiokoa ndipo aliposikia sauti ya mke wake ikimuita Edson, aliisikiliza sauti hiyo vizuri, bila kubahatisha, akagundua kwamba huyo alikuwa mkewe tu.
Alihisi kitu chenye ncha kali kiiuchoma moyo wake, maumivu aliyoyasikia hayakuelezeka, hakutaka kuishia kuisikia tu bali alichokifanya ni kupiga mbizi kuelekea kule aliposikia sauti ile, alipofika, hakuamini, alimuona mkewe, Anita akiwa ameshikwa vilivyo na Edson.
Hapohapo baharini machozi yakaanza kummwagika, alihisi maumivu makubwa ambayo hakuwahi kuyasikia hapo kabla. Hakutaka kuendelea kuona kile kilichokuwa kikiendelea, alichoamua ni kuanza kupiga mbizi kuelekea upande ambao hakujua kama ungekuwa salama kwake, alichokitaka ni kusonga mbele na kutoka katika uwepo wa mahali pale.
“Anita…unanifanyia hivi? Nimekukosea nini Anita?” aliuliza Phillip huku akiendelea kupiga mbizi.
Mawimbi yalimpiga, alipelekwa huku na kule lakini msimamo wake ulikuwa mmoja tu kwamba ni lazima afike kule alipokuwa akielekea kipindi hicho. Kujua kuogelea ilikuwa nafuu kwake, aliendelea kupiga mbizi mpaka alipofika mbali kabisa ambapo akahisi kuchoka, hakutaka kuendelea tena kwani mikono yote ilikuwa ikiuma. Alichokifanya ni kutulia tu.
Muda ulizidi kwenda, mpaka bahari ilipotulia kabisa, hakuweza kukisogeza kiungo chake hata kidogo na mbaya zaidi akaanza kupoteza fahamu, mawimbi yaliyokuwa yamempiga yalimchosha kabisa, akalegea na kuanza kuzama baharini, baada ya hapo, hakujua kilichoendelea kwani macho yalianza kujawa na giza, hakujua ni kitu gani kiliendelea.
Phillip aliporudiwa na fahamu, alishangaa kujikuta akiwa ndani ya nyumba moja, hakujua palikuwa wapi kwani hata nyumba yenyewe ilikuwa ni ya nyasi. Nje, mvua ilikuwa inanyesha na maji yake yalipita ndani kupitia mlangoni hali iliyoifanya sakafu ya nyumba ile kulowanishwa na maji, na kwa kuwa ilikuwa ni ya mchanga, tope likajaa ndani.
Phillip akainuka, akaanza kuangalia huku na kule, ndani hakukuwa na mtu hata mmoja ila ilikuwa ni mchana kwani hata mwanga wa nje ulikuwa ukipiga ndani kupitia sehemu zilizokuwa wazi.
Akaanza kukumbuka nini kilitokea mara ya mwisho alipopoteza fahamu. Alichokikumbuka ni kwamba alikuwa baharini akipiga mbizi kuelekea asipopafahamu, baada ya umbali fulani, alichoka, akatulia, akaanza kuzama na kisha kupoteza fahamu.
Hivyo ndivyo vitu alivyovikumbuka tu. Swali lililomsumbua kichwani ni juu ya mahali alipokuwa kipindi hicho.Akajitahidi kusimama palepale kitandani, akalisogelea dirisha na kuchungulia nje.
Alichokiona ni kwamba alikuwa ufukweni, pale alipokuwa, aliweza kuwaona watu wakiwaanika samaki wao, wengine wakiwatoa katika mitumbwi yao, mpaka hapo akajua kwamba watu waliokuwa wamemuokoa baharini walikuwa wavuvi.
Wala hakukaa sana, mara mlango ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuingia ndani. Alipomuona Phillip, uso wake ukajawa na tabasamu pana, hakuamini kama mwanaume huyo alifumbua macho yake.
“How do you feel?” (Unajisikiaje?) aliuliza mwanaume huyo aliyekuwa na mchanganyiko wa rangi.
“I am doing just fine…” (Najisikia vizuri) alijibu Phillip.
Alibaki akimwangalia mwanaume huyo, moyo wake ulikuwa na shauku ya kutaka kufahamu hapo alikuwa wapi na nini kilitokea baharini mpaka kufanikiwa kuokolewa. Kila alipomwangalia mwanaume yule, alijikuta akiingia hamu ya kutaka kufahamu kila kitu.
“Nitakueleza kila kitu, usijali,” alisema mwanaume yule ambaye alionekana kufahamu kilichokuwa kichwani mwa Phillip.
Akampa dawa na kunywa, baada ya hapo, akamletea chakula, Phillip akakichukua na kula kwa haraka sana, alikuwa na njaa kali, chakula kile alikila kwa haraka lakini hakushiba, akaongezewa kingine, nacho akala mpaka kukimaliza.
“Hapa ni wapi? Ilikuwaje mpaka nikawa hapa?” aliuliza Phillip.
Hapo ndipo mzee yule akaanza kumhadithia kila kitu kilichotokea. Phillip alibaki kimya akimsikiliza, alikuwa makini, hakutaka kupitwa na kitu chochote kile.
“Tulikuwa tunavua samaki kama kawaida yetu, baada ya kufika mbali, tukaona kitu kikielea juu ya maji, kwanza tulihofia kwani mara nyingi vitu kama hivyo huwa ni hatari kwetu.
“Nikawaambia wenzangu tusiogope, tukusogelee na tujue ni kitu gani. Walinikatalia lakini baada ya kuwalazimisha sana, wakakubaliana nami, hivyo tukakufuata.
“Ulionekana kuchoka sana, haukuwa na nguvu, tukakuchukua na kukuweka ndani ya mtumbwi na ndipo safari ya kuja hapa ilipoanza,” alisema mzee huyo.
“Na hapa ni wapi?”
“Hiki ni Kisiwa cha Comoro, hapa ni Mtsamboro,” alijibu mzee yule.
“Kwa hiyo wewe ni Mcomoro?”
“Hapana. Mimi na wenzangu ni watu wa Madagaska. Sisi ni wavuvi, tunakwenda kila sehemu kuvua. Baada ya hapa, tutarudi nyumbani kupitia Mliha na Mamoudzou kisha nyumbani,” alisema mzee yule.
Phillip akabaki kimya, akamwangalia mzee yule, moyoni mwake alishukuru kwani halikuwa jambo la kawaida mtu kunusurika baharini wakati boti imepata ajali na kuzama.
Baada ya kupewa muda wa kupumzika hapo ndipo mawazo juu ya familia yake yalipomjia kichwani. Picha ile aliyoiona baharini wakati mke wake, Anita alipokuwa akimuita mwanaume mwingine badala yake ikajirudia, moyo wake ukaumia mno na kugundua kwamba hatimaye mke wake aliamua kurudi kwa mpenzi wake wa zamani.
Hasira ikamkaba kooni, moyo wake ukavimba kwa hasira, kitu alichokiona kuwa kama kisasi kwa mke wake ni kumuua tu.
Walikaa hapo Mtsamboro kwa siku mbili na ndipo walipoanza safari yao ya kuelekea Madagaska kwa kupitia katika sehemu ambazo mzee huyo alimwambia Phillip kabla.
Kwa kuwa wao ndiyo waliomsaidia baharini, kila mmoja alimfahamu. Huko njiani walitumia siku tatu ndipo walipoingia Madagaska. Phillip hakutaka kurudi nchini Tanzania, alijua kwamba angeumia zaidi kama angemuona mkewe akitanua maisha akiwa na mwanaume mwingine.
“Ila walinusurika kweli? Isije ikawa nahofia kuonana naye kwa kisingizo cha kuumia na wakati walikufa baharini,” alijisemea Phillip.
Hakutaka kufuatilia kwa kipindi hicho, alichokifanya ni kusubiri. Baada ya kuishi siku mbili zaidi kisiwani Madagaska ndipo mzee yule alipomwambia kwamba kama angetaka kuishi kwa amani kisiwani hapo basi ingekuwa ni lazima kujiunga na jeshi la nchi hiyo.
Hiyo ilionekana kuwa ngumu kwake kwani hakuwa mtu wa kisiwa hicho. Sababu hiyo akamueleza mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mgege. Mzee huyo akamwambia kwamba hilo halikuwa tatizo kwani kulikuwa na watu wengi kutoka mataifa mengine waliokuwa wakijiunga na jeshi la Madagaska kwani nchi hiyo ilikuwa ndogo, hivyo kuchukua watu wengine kutoka nchi nyingine lilikuwa la kawaida.
Siku hiyo aliyokubaliana naye, akapelekwa mpaka katika makao makuu ya kijeshi ya nchi hiyo. Waliposikia kwamba Phillip alikuwa Mtanzania aliyekuwa radhi kujiunga na jeshi lao, walifurahi sana.
Watanzania walionekana kuwa tofauti na watu wengine, walijua kuongea, walijua kuanzisha vitu na watu ambao uwezo wao wa kufikiri ulionekana kuwa mkubwa, imani hiyo ndiyo iliyojengeka mioyoni mwa Wamadagaska wengi hali iliyowapelekea kumkubali Phillip bila kikwazo chochote.
Maisha mapya yakaanza, hakukuwa na mtu aliyejua historia ya maisha yake, wote walimchukulia mtu wao, mfa maji aliyetolewa baharini, kwa hiyo nyuma ya maisha tofauti na baharini, kulionekana giza kabisa.
Kambini, kila mwanajeshi alitaka kupiga naye stori, wengi walitaka kufahamu kuhusu hayati Julius Nyerere kwamba mkombozi wa nchi nyingi za Kiafrika, kila alipofika, watu walikusanyika na kuanza kumsikiliza.
Phillip alikuwa muongeaji mkubwa kiasi kwamba akapata marafiki wengi, wengi walimpenda na kuvutiwa naye.
Siku ziliendelea kukatika, mawazo juu ya mke wake yalimtawala, mchana alikuwa mzungumzaji mkubwa, watu walizifurahia stori zake lakini ilipofika usiku, alikuwa peke yake chumbani, mashavu yake yakalowanishwa na machozi kila alipomfikiria mke wake.
Alimpenda na kumthamini lakini picha ambayo aliiona usiku ilionyesha kwamba kama walipona katika ajali ile basi ilikuwa ni lazima watakuwa wakiishi pamoja, wakiyafurahia maisha na kutumia mali ambazo huyo Edson hakuwahi kuzitafuta hata mara moja.
Alichokifanya ni kuongeza juhudi jeshini, alipambana haswa, alifundishwa kutumia silaha, akapewa mazoezi makubwa ya kulenga shabaha. Hakukata tamaa, kila siku ilikuwa ni lazima kufanya mazoezi ya nguvu kiasi kwamba baada ya mwaka, akapewa V ya kwanza.
Hayo yalikuwa mafanikio makubwa, hakuishia hapo, aliendelea zaidi mpaka alipopata nyota ya tatu, akachukuliwa na kupelekwa katika kitengo cha usalama wa taifa ambapo huko, akapewa nyumba iliyokuwa jijini Antananarivo na maisha kuanza upya huku akilipwa mshahara mnono.
Yeye ndiye aliyekuwa na jukumu la kufanya ishu zote za mauaji. Kama kulikuwa na mtu ambaye alitakiwa kumalizwa haraka sana kwa maslahi ya taifa, alitumwa yeye na kazi kuifanya kwa umakini mkubwa pasipo kujulikana.
Mtaani, ilikuwa ni vigumu kujua kama Phillip alikuwa mtu wa usalama wa taifa, aliishi maisha ya kipole, kuzungumza na watu wengi huku akiwasaidia katika kazi nyingi za kijamii.
Miaka ikakatika tu, siku zikasogea mpaka alipofikisha miaka mitatu kisiwani Madagaska, akaomba nafasi ya kwenda nchini Tanzania, alitaka kuiona familia yake, wakuu wake wakakubaliana naye kwani alikwishawaambia historia ya maisha yake ilikuwa vipi, hivyo akaelekea huko.
Alipofika, hakutaka kugundulika, alijificha hotelini huku kila siku alipokuwa akitoka, alivaa kofia, miwani miyeusi na ndefu nyingi za bandia kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kugundua kwamba mtu huyo alikuwa Phillip.
Hapo ndipo alipoanza kwenda Mikocheni B kulipokuwa na nyumba yake. Mara baada ya kwenda huko, alisimama pembani mwa nyumba hiyo, mbali kabisa na kuanza kuiangalia.
Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama kila kitu kilichokuwa kimetokea kilibaki na kuwa historia. Kila siku ilikuwa ni lazima kwenda mtaani hapo kwa ajili ya kuangalia hali ilivyokuwa ikiendelea.
Aliona kwamba kama asingeweza kufanya kitu fulani kamwe asingeweza kufanikiwa kupata kile alichokitaka. Alichokifanya ni kwenda kwa jirani yake ambaye alizoeana naye sana, huyo alikuwa Emmanuel Kigomi, mfanyabiashara tajiri asiyekuwa na mtoto katika maisha yake baada ya kuharibika mfumo mzima wa uzalishaji mbegu.
Alipofika getini, akapiga hodi na mlinzi kumkaribisha. Kwa kumwangalia, hata mlinzi mwenyewe hakujua kama mtu aliyesimama mbele yake alikuwa Phillip. Akamuulizia Emmanuel, akaambiwa asubiri.
“Nimwambie nani?”
“Rafiki yake.”
“Anao wengi tu, nimwambie nani sasa? Au bwana madevu?” aliuliza mlinzi kwa sura iliyoonyesha alikuwa akitania.
“Mwambie jirani yake.”
Mlinzi akapiga simu ndani, simu ikapokelewa na mfanyakazi ambaye aliiunganisha mpaka chumbani kwa mzee huyo na kisha kupewa Phillip na kuzungumza naye.
“Unaweza kwenda pembeni kidogo?”
“Haina tatizo.”
Mlinzi akasogea huku akiwa na bunduki yake mkononi, akamwacha Phillip akizungumza na Emmanuel katika simu ile. Phillip alijitambulisha, Emmanuel hakuamini, aliuliza mara mbili kama mtu aliyekuwa akizungumza naye alikuwa Phillip kweli.
“Ndiye mimi.”
“Ila ulikufa!”
“Uliuona mwili wangu kwenye jeneza?”
“Hapana.”
“Basi jua kwamba nipo hai.”
“Ilikuwaje kwanza?”
“Ndiyo nataka nije nikuhadithie, pia ningehitaji msaada kutoka kwako.”
“Wa kifedha? Hakuna tatizo.”
“Hapana Emmanuel, sihitaji msaada wa kifedha, si unanijua kwamba nina fedha za kutosha, nataka msaada wa mambo fulani,” alisema Phillip.
“Basi hakuna noma, njoo.”
Alichokifanya Phillip ni kumpa simu mlinzi ambaye aliambiwa amruhusu mgeni huyo kuingia. Phillip akaingia mpaka sebuleni na macho yake kukutana na Emmanuel. Mwanaume huyo hakuamini kama aliyesimama mbele yake alikuwa Phillip, alikuwa na muonekano wa tofauti kabisa, wakakumbatiana na kukaa kochini.
“Kwanza niambie kuhusu mke wangu!”
“Unataka kujua nini?”
“Anaendeleaje? Yupo peke yake kweli?” aliuliza Phillip.
Emmanuel akainamisha kichwa chini, alionekana kuguswa na swali hilo, alionekana kufahamu kitu lakini hakutaka kumwambia Phillip kile kilichokuwa kikiendelea kwa kuamini kwamba mwanaume huyo angeumia.
“Niambie kila kitu, usinifiche, mpaka kuja kwako jua kwamba ninakuamini,” alisema Phillip.
“Ukweli ni kwamba mkeo ana mwanaume mwingine,” alisema Emmanuel.
“Anaitwa Edson, si ndiyo?”
“Umejuaje?”
Hapo ndipo Phillip alipoanza kumhadithia Emmanuel kile kilichotokea kwenye boti wakati wakiwa safarini kuelekea Unguja. Hakuficha kitu, alihadithia kila kitu tangu walipokutana na mwanaume aliyetambulishwa kwa jina la Edson ambaye alikuwa amepigwa sana na maisha.
Hakuishia hapo, aliizungumzia ajali iliyotokea mpaka alipookolewa na wavuvi kutoka Madagaska. Kila alipohadithia na kulitaja jina la mke wake, alionekana kuumia sana.
“Pole sana kwa yaliyotokea.”
“Asante sana. Sasa unaweza kuniambia chochote unachojua,” alisema Phillip.
“Kuna mengi ila kwa kifupi ni kwamba jamaa ana lengo la kumuumiza mkeo, anaingiza wanawake tofautitofauti, ni mlevi kupindukia, ila la zaidi kabisa, tetesi za mtaani zinasema kwamba jamaa anataka kumtapeli mali zote mkeo kwani amemwandika katika mali zote,” alisema Emmanuel.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Hivyo ndivyo ninavyovifahamu.”
“Unahisi kwamba atafanikiwa katika dhamira zake?”
“Kama zipi?”
“Kumtapeli mali?”
“Kwa nini asiweze.”
“Hawezi kwa kuwa kila kitu ninacho, alivyokuwa navyo Anita ni batili,” alisema Phillip.
“Kweli?”
“Amini hilo. Ila ninataka kuona jinsi mchezo utakavyokuwa, kuna mengi nitafanya,” alisema Phillip huku akionekana kukasirika.
*****
Ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ndicho alichokifanya. Phillip hakutaka kurudi Madagaska, aliwasiliana na wakuu wake na kuwaeleza kila kitu kilichokuwa kimetokea hivyo ilikuwa ni lazima akamilishe kazi zote na ndipo arudi huko kuendelea na kazi.
Hakukuwa na mtu aliyemtilia mashaka, walimwamini kwa kuwa alikuwa mtu wa kujitoa sana na kitu cha pili ambacho kiliwapa ugumu wa kumzuia ni kwamba alikuwa nchini mwake.
Alichokifanya Phillip ni kwenda kupanga chumba maeneo ya Tandale, chumba cha bei ya chini ambapo huko akaanza kazi ya kuokota chupa za maji. Ilikuwa ni kazi ngumu lakini kwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa mpelelezi tangu alipokuwa Madagaska, hivyo kazi hiyo haikuwa na ugumu wowote ule.
Alizunguka sehemu nyingi jijini Dar es Salaam lakini sehemu kubwa ambayo alipendelea kwenda ni kule kulipokuwa na nyumba yake, Mikocheni B. Alipofika huko, hakukuwa na mtu aliyemtambua, alikuwa na ndevu chafuchafu, nguo zilizochakaa na hata mlinzi wake alipomuona, hakugundua kwamba huyo alikuwa Phillip.
“Vipi kaka?” alisalimia mlinzi.
“Poa. Karibu.”
“Asante. Nimekuja kupekuapekua ili nione kama naweza kupata ridhiki,” alisema Phillip.
“Daah! Takataka zipo kule nyuma.”
“Niruhusu tu kaka, si unajua nyie hamnywaji maji ya bomba, nyie na chupa za maji tu,” alisema Phillip.
Mlinzi alimwangalia, alionekana kweli kuwa mtu mwenye uhitaji, alichokifanya ni kumruhusu na Phillip kuingia ndani. Alikwenda moja kwa moja kulipokuwa na pipa la takataka na kuanza kulipekua huku akizitafuta chupa za maji.
Alipozikuta, akazichukua na kuelekea getini ambapo alimkuta mlinzi akimsubiri. Alichokifanya ni kumshukuru.
“Asante sana.”
“Poapoa. Kuna kingine?”
“Au kama mtataka nifanye hata kazi za kubeba takataka kwani naziona kuwa nyingi mno,” alisema Phillip.
“Ngoja nizungumze na shemeji.”
Mlinzi yule akaondoka kuelekea ndani, ndani ya dakika chache akarudi huku akiwa ameongozana na Anita. Alipomuona, mapigo ya moyo wake yakaanza kudunda kwa nguvu, hakuamini kama yule aliyesimama mbele yake alikuwa mke wake.
Mwili wake ulionekana kupungua kutokana na mawazo, alishindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumlengalenga huku moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali kiasi kwambam kuendelea kujifanya muokota chupa za maji ilihitaji moyo.
“Za saa hizi dada…” alimsalimia.
“Salama. Karibu.”
“Asante. Nilikuwa nahitaji niwe nabeba takataka hapa kwako,” alisema Phillip.
“Tena afadhali umekuja, hili gari siku hizi linachelewa sana, utakuwa unatubebea kwa kiasi gani?”
“Pipa zima hata shilingi elfu mbili, hakuna tatizo.”
“Basi sawa. Nitakuwa nakupa elfu tano kabisa.”
“Nashukuru sana,” alisema Phillip huku akikiinamisha kichwa chake kama kutoa shukrani.
Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba yule aliyesimama mbele yao alikuwa Phillip. Alijibadilisha vya kutosha, alionekana kama masikini fulani ambaye aliyahangaikia maisha yake kila siku.
Hata mkewe ambaye aliishi naye kwa miaka sita, hakugundua kwamba yule alikuwa mume wake, aliongea naye mpaka alipomruhusu na kuondoka, hakuwa amejua kabisa.
Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake, kila wiki ilikuwa ni lazima kufika hapo nyumbani, anachukua chupa za maji na siku nyingine kwenda kubeba takataka zilizokuwa kwenye pipa.
Mlinzi akatokea kumzoea ana Phillip aliyejitambulisha kwa jina la Kizota, wakawa marafiki wakubwa, na hata siku ambayo Phillip alipokuwa akienda huko ilikuwa ni lazima kuwasiliana na mlinzi.
Kila walipokutana, stori zao walizokuwa wakipiga ni za mpira tu. Pamoja na kuonekana kuwa masikini wa kutupwa lakini wakati mwingine maongezi aliyokuwa akiongea Phillip yalimshangaza sana mlinzi, alionekana kuwa na uwezo mkubwa sana kichwani mwake, mambo aliyoongea yalikuwa na maana kubwa.
“Unapozaliwa, unakuwa hauna kitu kabisa, si ndiyo?” aliuliza Phillip.
“Ndiyo!”
“Huo si ujinga wako Abrah! Ukiona mtu kazaliwa masikini, usimcheke na kumtukana kwa nini kazaliwa masikini,” alisema Phillip.
“Kumbe…”
“Ndiyo! Mcheke mtu kama kafa akiwa masikini. Tunapozaliwa huwa hatuna kitu katika maisha yetu, tunapambana usiku na mchana ili tupate kitu, tazama matajiri wengi, ni wachache mno ambao wamezaliwa kwenye familia zenye hela.
“Wengi wamezaliwa kwenye familia masikini. Mwangalie Bakhresa, Bill Gates na wengine, hawakuwa na kitu hapo nyuma ila sasa hivi, wana fedha, wana kila kitu,” alisema Phillip.
“Ndiyo maana tunatafuta.”
“Sikiliza Abrah! Ni vigumu kupata utajiri ukiwa chini ya mtu. Huwezi kufanikiwa zaidi ukiwa umeajiriwa, ni lazima akili yako ichaji, ujue ni kwa namna gani unaweza kuingiza fedha. Anzisha biashara zako, usiwe na mlango mmoja wa kuingiza fedha, hakikisha unakuwa na milango hata mitatu, hapo ndipo utakapoona mafanikio yako,” alisema Phillip.
“Ebwana! Unajua wewe kuwa muokotaji wa chupa za maji siyo haki kabisa,” alisema mlinzi.
“Kwa nini?”
“Ungekuwa profesa sasa hivi! Una maneno mazito sana ambayo ni faida kwa kila mtu,” alisema mlinzi.
Kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo walivyoendelea kuzoeana zaidi. Usiri mkubwa ulikuwepo baina ya Phillip na Emmanuel, mwanaume huyo hakutaka kumwambia mtu yeyote kwamba Phillip alikuwa hai, kila kitu kilichokuwa kimetokea kwake kilikuwa siri nzito.
Baada ya kuzoeana kwa kipindi cha miezi sita ndipo alipoanza kumdadisi mlinzi juu ya maisha ya mkewe na Edson ndani ya nyumba hiyo. Kwa kuwa mlinzi ilifika kipindi alimwamini sana Phillip, akaamua kumwambia mengi tu.
“Mwanaume anazingua sana, kutwa kuingiza wanawake, anakula bata sana, nafikiri kwa sababu mali hakuzitafuta kwa nguvu zake,” alisema mlinzi.
“Kwani mali si zake?”
“Thubutuuuu…mali za marehemu mume wa Anita. Alikufa baharini, baada ya hapo Anita akawa na huyu mwanaume mpaka ndugu zake wakashangaa….” alisema mlinzi.
“Kwa nini washangae?”
“Ilikuwa mapema mno, ila yeye hakujali.”
“Ila kuna vijitetesi nimevisikia kwa jirani nilipokwenda kuokota chupa.”
“Vipi?”
“Kwamba huyu jamaa anataka kumtapeli mali hizi mwanamke!”
“Hizo si tetesi. Kesho wateja wanakuja kwa ajili ya kununua nyumba hii.”
“Acha masihara.”
“Sasa nikutanie ili iweje Kizota. Yaani kila ninapomwangalia shemeji, siamini, ananyanyasika sana, hana mbele wala nyuma, badala ya mapenzi sasa imekuwa ni maumivu usiku na mchana,” alisema mlinzi.
Mlinzi hakuishia hapo, aliendelea kumwaga umbeya, katika mazungumzo yake akawataja mabilionea ambao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Phillip anapata mali hizo.
“Wakina nani?”
“Kuna mmoja alikuwa hakimu, huyu anaitwa James Marimba na mwingine mfanyabiashara anaitwa Andrew Nkone,” alisema mlinzi.
“Mmh! Kweli kazi ipo. Pole yake.”
Phillip hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka kuelekea nyumbani kwake. Njiani, hasira zilimkamata kooni, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea.
Alimkumbuka mkewe, mtoto wake ambao kwake walikuwa kila kitu, hakuamini kama Edson, yuleyule mwanaume mchafu aliyeonekana kupigwa na maisha ndiye ambaye alitaka kujimilikishia kila kitu ambacho alikitafuta kwa jasho lake.
Japokuwa utapeli ulitaka kufanyika lakini kwake halikuwa tatizo kubwa, alijua kwamba hati alizokuwa nazo mkewe hazikuwa zenyewe bali zilikuwa za kugushi ambazo kwa kuziangalia zilionekana kuwa zenyewe.
Kesho yake alipoingia, akaambiwa na mlinzi kwamba watu hao walikuwa ndani tayari kwa kukamilisha kila kitu kuhusu kuuzwa kwa nyumba hiyo. Wakati wanazungumza hayo, hawakukaa sana, Anita akafika nyumbani hapo, alionekana kuwa na haraka huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.
Hakuzungumza kitu chochote kile, akaingia ndani. Phillip na mlinzi hawakutaka kubaki mahali pale, walisogea mpaka karibu na dirisha na kuanza kusikiliza huko ndani ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea.
Walimsikia Anita akimlalamikia Edson kwamba alitaka kuuza nyumba hiyo huku kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimetolewa katika akaunti yake na kuachiwa milioni tano tu.
Phillip alinyong’onyea, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, wakati mwingine alitamani kuingia ndani na kuwaambia watu hao kwamba alikuwa Phillip na hakuwa radhi kuona mali zake zikiuzwa.
“Unasikia, kimeshanuka humo ndani, nyumba inauzwa,” alisema mlinzi huku wakitegesha masikio kusikia vizuri.
*****
Alichokitaka Phillip ni kuanza kufanya upelelezi wake, alitaka kuwafahamu watu ambao walitajwa na mlinzi kwamba ndiyo waliokuwa wakishirikiana na Edson Kambani kwa ajili ya kumtapeli mke wake mali zile.
Akaanza kufanya uchunguzi, mtu wa kwanza aliyetaka kumfahamu kwa undani alikuwa James Marimba. Alikumbuka kwamba aliambiwa kuwa mtu huyo alikuwa hakimu hapo mwanzo, hivyo akataka kufuatilia alikuwa hakimu wa wapi na kwa namna gani alizipata fedha zake na kuwa bilionea mkubwa.
Alichokifanya ni kuanza kumfuatilia kupitia Google, humo, akagundua kwamba alikuwa hakimu mkazi wa mahakama moja jijini Dar es Salaam. Hakuridhika, alitaka kufuatilia zaidi, akagundua mpaka sehemu alipokuwa akiishi kwa wakati huo, katika jumba moja lililokuwa Msasani.
Ufuatiliaji wake haukuishia katika mitandao tu bali kwenda mpaka alipokuwa akiishi mzee huyo. Ilikuwa nyumba kubwa, ndani kulikuwa na mfanyakazi mmoja na pia familia yake ya mke mmoja na watoto wawili.
Aliendelea na uchunguzi wake, akagundua kwamba watoto wa mzee huyo walikuwa wakisoma St. Anne Marie iliyokuwa Kipawa na mke wake alikuwa mkurugenzi wa kampuni yao changa iitwayo Wood Forest Marimba Company iliyokuwa ikijishughulisha na usambazaji mbao baada ya kukata miti porini.
Alipomaliza kumfuatilia bwana Marimba, akaanza kumfuatilia na Andrew Nkone. Akagundua kwamba mzee huyo alikuwa tajiri mkubwa aliyevuna fedha kupitia kampuni zake mbili, moja ikiwa ni ya kutengeza mabati na nyingine juisi.
Nyumbani, alikuwa na mke mmoja na watoto wanne. Mbali na fedha zake, mke wake mzuri lakini bwana Nkone alikuwa mtu wa kutoka sana nje ya ndoa. Alikuwa na vimada viwili, wa kwanza alikuwa Upendo, msichana aliyempangia nyumba maeneo ya Magomeni na mwingine aliitwa Sikitu ambaye pia alimpangia nyumba maeneo ya Kimara Suka.
Upelekezi wake ulipokamilika, akaanza kuwa na jukumu la kuilinda familia yake kwani alijua kwamba ilikuwa ni lazima mkewe afukuzwe nyumbani na baada ya hapo kuanza kutafutwa kwa lengo la kuuawa.
Alichokuwa amekifikiria ndicho kilichotokea, baada ya siku kadhaa, Anita akafukuzwa nyumbani kwake na hivyo kuelekea kwa wazazi wake. Binti yake aliyekuwa akisoma katika shule za kitajiri, akafukuzwa na kuanza kusoma shule za uswahilini.
Aligundua kwamba huo usingekuwa mwisho, hivyo alichokifanya ni kurudi Madagaska kisha kuwatuma vijana ambao wangefuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea na baada ya miaka kadhaa ndipo alipoanza kuagiza kufanywa baadhi ya matukio ambayo yalikuwa na lengo la kuilinda familia yake.
*****
Kilichotokea, vijana hao waliotumwa nchini Tanzania waliweza kufanya majukumu yao yote, walifanikiwa kumlinda Anita na mtoto wake kwa kuwaua vijana wote waliotumwa na mabilionea wale kisha kumchukua mtoto Cynthia na kuondoka naye kuelekea Madagaska.
Katika kipindi ambacho Cynthia alifikishwa nchini humo, Phillip hakuamini, kila alipomwangalia mtoto wake, machozi yalikuwa yakimtoka tu. Kilipita kipindi kirefu hakuwa amemuona, kitendo cha kumuona kwa mara nyingine kilimpa furaha kubwa.
Cynthia hakujua kama yule ni baba yake, aliondoka nchini Tanzania akiwa mtoto mdogo kabisa, miaka miwili. Alimwangalia mtu aliyesimama mbele yake, kwa mbali alihisi kufanana naye lakini kila alipojaribu kuvuta kumbukumbu kama aliwahi kumuona sehemu fulani, hakukumbuka chochote kile.
Phillip akamchukua Cynthia, akampakiza ndani ya gari na kuanza kuondoka naye. Muda wote huo Cynthia hakuzungumza kitu, alimshangaa mtu aliyekuwa naye, alikuwa akitokwa na machozi lakini hakujua sababu haswa ilikuwa nini.
Kichwa cha Cynthia kilikuwa na maswali mengi, hakutaka kuuliza, alibaki kimya huku akimwangalia baba yake tu. Safari ile iliishia nje ya jengo moja kubwa na la kifahari, kwa jinsi alivyoliangalia jumba lile hakuamini kama na yeye angeweza kuingia humo.
Geti likajifungua na kuingia ndani. Watu zaidi ya watano waliokuwa na bunduki walikuwa wakizunguka huku na kule. Ulionekana kuwa ulinzi mkubwa kitu kilichomfanya kujiuliza juu ya mtu huyo aliyekuwa amemchukua.
Gari lilipopakiwa sehemu ya maegesho, wote wawili wakateremka na kuelekea ndani. Cynthia alionekana kuwa huru, alimwamini mtu huyo kwani watu ambao walimchukua nchini Tanzania alizungumza nao na kumwambia kwamba angekuwa salama.
“Unahitaji nini?” aliuliza Phillip huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Nataka chakula.”
Hapohapo Phillip akamuita mfanyakazi wa ndani na kumwambia amletee chakula, kwa haraka, chakula kikaletwa na kuanza kula, alipomalizwa, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kimoja kilichoonekana kuwa na mvuto mkubwa.
“Unajua mimi ni nani?” aliuliza Phillip.
“Hapana!”
“Hujawahi kuniona?”
“Hapana!”

ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA

Facebook Comments

Tags
Show More

Related Articles

Close