Life Style

Kweli Ni muhimu kuzaa, lakini unazaa na Nani?

KADIRI miaka inavyozidi kuyoyoma, wimbi kubwa la wanawake kutaka kuzaa limezidi kuongezeka. Hii inatokana na suala zima la umri. Mwanamke akiona umri unamtupa mkono, haraka sana anahaha kusaka mtoto. Utasikia; ‘bora na mimi hata nizae tu niache angalau chata hapa duniani.’

Suala hili pia lipo kwa wanaume lakini kwa asilimia kubwa linawatesa sana wanawake. Wanapoona miaka inakatika, wanakimbilia kuzaa bila hata ya kuangalia anazaa na nani. Anazaa tu ili mradi naye aitwe mama.

 

Wapo wengi ambao sasa hivi pia wanaamua kuzaa kwa kufuata mtindo wa sasa kwamba hawataki stress. Mwanamke anasaka maisha yake, anaona anajimudu hivyo hataki kushirikiana na mwanaume sababu atamuongezea matatizo. Sasa hivi wengi najua ni mashahidi wa hili.

Wanawake wengi ukizungumza nao, wanakuambia hawataki kuishi na mwanaume. Wanasema eti ni wasumbufu na wao hawataki usumbufu. Hivyo anaamua kuzaa na mwanaume ambaye hata hana mwelekeo wowote wa maisha. Ili mradi tu ampatie mtoto halafu yeye andelee na maisha yake.

Hataki kusikia habari za kubanywa na mwanaume kwamba uko wapi, unafanya nini au kwa nini umechelewa kurudi nyumbani. Anataka ashindane na wanaume wanaochelewa kurudi nyumbani kutokana na majukumu mbalimbali ya kikazi.

 

Akiamua kurudi nyumbani alfajiri, sawa! Kifupi ni kwamba wanawake wanataka uhuru. Wanahitaji nafasi, hawataki kubanwabanwa na wanaume. Wanahitaji nafasi. Wanahitaji kufanya maamuzi yao bila kubughudhiwa na mtu. Hiyo ni kampeni ambayo imeanza taratibu miaka ya nyuma lakini kwa sasa, imepenya vilivyo kwenye bongo za wanawake na wengi wao huwaambii kitu kuhusu wanaume. Yeye ni mwanamke lakini anajiona hana tofauti na mwanaume. Ana nyumba yake, ana usafiri wake ana kila kitu, utamueleza nini. Mwanamke anakuambia amnyenyekee mwanaume wa nini? Kama ni uwezo wa kutafuta anao, hicho ndicho kizazi cha sasa. Mwanamke naye anaamua azae na nani.

 

Akishazaa naye, mtoto wake anamlea mwenyewe. Hahitaji msaada wowote kutoka kwa huyo mwanaume. Tena mara nyingi wanawake wa aina hiyo, wanataka wanaume ambao watawamudu. Wanaume ambao watawasikiliza. Kifupi ni kwamba mwanaume mpe mtoto, endelea na maisha yako. Mtoto si wako tena bali ni wake.

 

Atajua mwenyewe atamlea vipi sababu hataki kubanywabanywa. Marafiki zangu, kwa namna yoyote ile ni vyema sana licha ya kutaka watoto Lakini ni vyema kuangalia unazaa na nani. Nasema hivi kwa sababu ili kutengeneza kizazi kizuri ambacho kitalelewa na wazazi wote wawili, ni vyema sana kujua mtu sahihi ambaye utazaa naye. Zaa na mtu ambaye unaamini mtalea pamoja familia.

 

Mtu ambaye mtalea naye hao watoto maana watoto wa kulelewa na upande mmoja nao wanakuwa na changamoto ya kukosa maadili. Tunawaona watoto ambao wanalelewa na upande mmoja, madhara yake tunatengeneza kizazi cha vijana wahuni, wavuta bangi na hata kuwa majambazi. Hata kama umechelewa kuzaa, hakikisha unazaa na mtu sahihi ambaye mtafanya naye maisha na ikiwezekana kufunga ndoa naye kwani hakuna anayesema kwamba binadamu ni lazima uolewe au kuoa ukiwa na umri fulani, muda muafaka ni ule ambao nyinyi mtaamua kuoana.

Facebook Comments

Tags
Show More
Close